vituo vidogo vya mafuta kuanzishwa vijijini

Sarah Moses, Dodoma.

SERIKALI kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA),imetangaza kuanza usambazaji wa vituo vidogo vya mafuta vijijini.

Hayo ameyasema leo Agosti  18  Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji  wa majukumu ya wakala huo na mwelekeo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Amesema kuwa usambazaji wa Mradi huo unahusu kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya kusambaza bidhaa za mafuta katika maeneo mbalimbali ya vijijini.  

Mradi wa utoaji Mikopo ya Ujenzi na Uendeshaji wa Vituo Vidogo vya mafuta ya Petroli na Diseli vijijini Tanzania bara, ambapo amesema lengo kuu ni kulinda mazingira na afya ya watumiaji na kuboresha upatikanaji na usambazaji wa Mafuta vijijini.

“Kiasi cha mwisho cha mkopo ni Shilingi 75,000,000;

ambapo riba yake ni asilimia 5 , kwa muda wa marejesho ya miaka 7″ amesema.

Kwa mwaka 2023/24 kiasi cha shilingi bilioni 10 kimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo nafuu kwa waendelezaji ambapo kwa sasa wakala unaendelea kupokea maombi ya waombaji, huku mwisho wa kupokea maombi ni 25 Agosti 2023.

Pamoja na hayo amesema kuwa Serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB), imetenga Dola za Marekani milioni 6 kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa majiko banifu ya kupikia ambapo takribani majiko 200,000 yanatarajiwa kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya vijijini na vijiji miji Tanzania bara. 

“Wanufaika wa mradi huo ni wazalishaiji na wasambazaji wadogo wa ndani wa majiko banifu,ambapo lengo la mradi huo ni kukuza na kuboresha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ambapo kwa sasa, Wakala upo kwenye mchakato wa uandaaji wa taratibu na kanuni za utoaji wa ruzuku hizo” amesema.

Kwa upande wa miradi iliyopo nje ya mfumo wa gridi, Mkurugenzi huyo amesema REA imesaidia miradi ya kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji Vituo Vidogo takriban 54 na mifumo ya kuzalisha umeme kwa jua takriban 30 ambayo kwa ujumla inazalisha takriban Megawati 38.

“Ndani ya mwaka wa fedha 2023/2024, tutaisaidia miradi 11 kwa ajili ya kuzalisha au kupeleka umeme kwenye maeneo ya vijijini nje ya mfumo wa Gridi ya Taifa. Kwa kiasi kikubwa zinatumika fedha za ndani japo pia tunapata misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo” amesema Mhandisi Saidy.

Mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *