Na Daniel Mbega, Dar es Salaam
MIFUGO na Uvuvi ni sekta nyeti katika uchumi wa nchi, ambayo ni pacha na sekta ya kilimo kutokana na umuhimu wake, siyo tu katika kuchangia uchumi, lakini pia inahusu uhakika wa akiba ya chakula.
Zaidi ya hayo, sekta hizo – kilimo, mifugo na uvuvi – kimsingi ndizo zinazoongoza kutengeneza fursa za ajira nchini Tanzania, ambako asilimia takriban 75 wanajishughulisha na kilimo, ikiwemo ufugaji na uvuvi.
Sera nzuri, mazingira bora na mkakati wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha uchumi unakua, ikibidi kufikia kwenye kiwango cha uchumi wa kati wa juu, vinaleta dalili njema ya kushamiri wa sekta hizi.
Ndiyo maana, katika mkakati wake wa kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake, akaanzisha Mpango wa Jenga Kesho Yako iliyo Bora (BBT), akihamasisha kilimo cha umwagiliaji.
Suala la mifugo na uvuvi ni moja ya vipaumbele vikubwa vya Rais Samia, ambaye amekuwa akihamasisha pia ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba.
Katika mwaka 2024/2025, serikali imetenga Shs. 363,118,170,000 kati ya Shs. 460,333,602,000 zilizopitishwa kwenye Bajeti ya Mifugo na Uvuvi, kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Fedha hizo zikitolewa kwa wakati zitafanikisha utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali, ambayo kufanikiwa kwake kutaipaisha sekta ya mifugo na uvuvi nchini.
Katika utekelezaji huo, viko vipaumbele takriban 25 ambavyo vimepangwa kwa mwaka huu wa fedha 2024/25, 15 vikiwa katika sekta ya mifugo na 10 katika sekta ya uvuvi.
Vipaumbele vilivyoko kwenye sekta ya mifugo ni; Kufanya kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo kwa kutoa chanjo kwa magojwa 13 ya kipaumbele; na Kukamilisha kuundwa kwa chombo maalum kitakacho simamia uendelezaji wa mazao na miundombinu ya mifugo.
Vipaumbele vingine ni; Kuanza kutekeleza Mradi wa Mageuzi katika Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (T-CSDTP) wa miaka mitano (5) wenye kunufaisha walengwa 58,000. Mradi utahusisha kununua ng’ombe wa maziwa 17,200; kujenga mabanda 5,000 ya ng’ombe; kujenga mfumo wa uvunaji maji ya mvua katika kaya 22,400; kununua na kusanikisha mitambo 2,800 ya biogesi; kujenga vituo 950 vya kukusanya maziwa; kununua dozi 929,000 za chanjo za mifugo; na kujenga kilomita 140 za barabara.
Aidha, vipaumbele vingine ni pamoja na Kuanzisha kambi moja ya Mifugo (Livestock Guest house) katika Ranchi ya Mkata; Kununua na kusambaza madume 60 ya mbari bora za mifugo aina ya Brahman ili kuongeza uzalishaji na tija katika mnyororo wa thamani wa mifugo na mazao yake; na Kujenga kituo cha mafunzo ya wadau wa mnyororo wa thamani wa malisho aina ya mabingobingo (Juncao).
Serikali pia imepanga Kuboresha na kuendeleza hekta 20,000 za maeneo ya malisho katika eneo la Msomera, Kitwai na Saunyi; Kukamilisha ujenzi wa mabwawa saba na visima virefu vitatu; Kuwezesha uendeshaji wa mashamba ya kuzalisha malisho na mbegu za malisho; na Kuwezesha FETA na LITA kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.
Hali kadhalika, Serikali kupitia wizara hiyo imepanga Kuziwezesha LITA na FETA kutekeleza Programu ya elimu na ujuzi wa kazi za uzalishaji (Education and Skills for Productive Jobs Program-for-Results – Phase II); Kuwezesha mradi wa Maziwa Faida TALIRI Tanga na African Dairy Genetic Gain katika mikoa saba nchini; Kuiwezesha TALIRI na TAFIRI kufanya tafiti mbalimbali; Kukarabati miundombinu ya kituo cha karantini cha Kwala ili kuwezesha biashara za kimataifa; na Kuzalisha chanjo za mifugo kupitia Wakala ya maabara ya Veterinari (TVLA).
Kwa upande wa Sekta ya Uvuvi, miradi itakayotekelezwa ni; Kukamilisha ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa – Masoko na kufanya maandalizi ya awali ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Bagamoyo; Kukamilisha uanzishaji wa chombo cha kusimamia na kuendeleza rasilimali za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji; na Kuendelea na taratibu za ununuzi wa Meli nne za uvuvi wa Bahari Kuu kupitia TAFICO.
Miradi mingine ni; Kujenga kiwanda cha kuchakata mazao ya uvuvi na kiwanda cha kuzalisha vyakula vya samaki; Kuwezesha ununuzi wa boti 450 na zana za uvuvi kupitia dirisha la ECF na Mradi wa TASFAM; Kuwezesha vikundi 300 kwa ajili ya kilimo cha mwani, ufugaji wa kaa na majongoo bahari; na Kununua meli moja ya mafunzo ya uvuvi kupitia mradi wa TASFAM.
Aidha, miradi mingine ni; Kununua maboya 60, ndege saba zisizo na rubani (drones) na kusanikisha mfumo wa ufuatiliaji wa vyombo vya uvuvi; Kuwezesha ununuzi wa vizimba 497 kupitia ECF; na Kuanzisha mashamba darasa 20 ya ukuzaji viumbe maji katika Halmashauri 20.
Kukamilika kwa miradi hiyo muhimu kutaongeza uzalishaji wa mifugo na uvuvi, ikiwemo mazao yake, kuliko ilivyokuwa katika mwaka uliotangulia.
Kwa hali halisi, katika mwaka 2023/2024, idadi ya mifugo nchini imeongezeka kutoka ng’ombe milioni 36.6 hadi ng’ombe milioni 37.9, mbuzi kutoka milioni 26.6 hadi milioni 27.6, na kondoo kutoa milioni 9.1 hadi milioni 9.4.
Aidha, kuku wameongezeka kutoka milioni 97.9 hadi milioni 103.1 ambapo kuku wa asili wameongezeka kutoka milioni 45.1 hadi milioni 47.4, kuku wa kisasa wameongezeka kutoka milioni 52.9 hadi milioni 55.7 na nguruwe wameongezeka kutoka milioni 3.7 hadi milioni 3.9.
Inaelezwa kwamba, Sekta ya Mifugo kwa mwaka 2022 ilikua kwa asilimia 5 na kuchangia asilimia 6.7 kwenye Pato la Taifa.
Taarifa ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi inasema kwamba, hadi kufikia Aprili, 2024, jumla ya ng’ombe 2,957,724 na mbuzi na kondoo 2,828,248 wenye thamani ya Shs. trilioni 3.4, waliuzwa katika minada mbalimbali hapa nchini ikilinganishwa na ng’ombe 2,218,293 na mbuzi na kondoo 2,121,187 waliokuwa na thamani ya Shs. trilioni 1.7 waliouzwa katika mwaka 2022/2023.
Ongezeko la idadi ya mifugo iliyouzwa minadani, kwa mujibu wa waziri mwenye dhamana, Abdallah Ulega, limetokana na kuongezeka kwa mahitaji ya nyama katika soko la ndani na nje ya nchi pamoja na hamasa ya uvunaji wa mifugo.
Akilihutubia Bunge wakati wa kuwasilisha bajeti ya wizara hiyo, Ulega alisema kwamba, katika mwaka 2023/2024, jumla ya vifaranga vya kuku 95,584,347 vimezalishwa na kusambazwa nchini ikilinganishwa na jumla ya vifaranga 83,845,967 vilivyozalishwa mwaka 2022/2023, sawa na ongezeko la asilimia 12.3.
Kati ya vifaranga hivyo, vifaranga vya kuku wa nyama ni 73,481,572; chotara 14,163,396; na kuku wa mayai 7,939,379; ikilinganisha na vifaranga vya kuku wa nyama 64,457,555; chotara 12,424,064 na kuku wa mayai 6,964,348 kwa mwaka 2022/23.
Lakini akasema, uzalishaji wa mayai umeongezeka kutoka mayai bilioni 5.50, mwaka 2022/2023 hadi mayai bilioni 6.41, mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 16.55.
Ongezeko hilo limesababishwa na kuimarika kwa vituo 28 vya kutotolesha vifaranga vya kuku vilivyopo nchini, mashamba 25 ya kuku wazazi, kuongezeka kwa ufugaji wa kuku wa mayai na hatua mbalimbali ambazo zimeendelea kucukuliwa za kudhibiti uingizaji holela wa vifaranga kutoka nje ya nchi.
Aidha, alisema, uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita bilioni 3.60, mwaka 2022/2023, hadi kufikia lita bilioni 3.97, mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 10.3 ambapo kati ya lita hizo, lita milioni 34.69 zimetokana na maziwa ya mbuzi na lita bilioni 3.93 zimetokana na maziwa ya ng’ombe, miongoni mwa hizo, lita bilioni 2.64 zinatokana na ng’ombe wa asili na lita bilioni 1.30 zimetokana na ng’ombe wa maziwa walioboreshwa.
Alibainisha pia kwamba, usindikaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita milioni 77.90, mwaka 2022/2023, hadi kufikia lita milioni 81.80, mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 5.01.
Pia, ukusanyaji wa maziwa kupitia vituo vya kukusanyia maziwa, umeongezeka kutoka lita milioni 71.80, mwaka 2022/2023, hadi kufikia lita milioni 93.40, mwaka 2023/2024.
Kama alivyosema Waziri Ulega, ongezeko la uzalishaji wa maziwa limechangiwa na utoaji elimu ya ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa kibiashara hapa nchini, kuongezeka kwa ng’ombe wa maziwa walioboreshwa pamoja na vituo vya kukusanyia maziwa vilivyofikia 258 mwaka 2023/2024 kutoka 246 mwaka 2022/2023.
Lakini si hivyo tu, Waziri Ulega alisema, hadi kufikia Aprili, Sekta ya Uvuvi imezalisha jumla ya tani 472,579.34 za mazao ya uvuvi. Kati ya hizo, tani 429,168.39 ni kutoka maji ya asili na tani 43,410.95 ni kutoka ukuzaji viumbe maji.
Akaongeza kuwa, uzalishaji wa mazao ya ukuzaji viumbe maji umefikia tani 43,410.95 kutoka tani 33,525.46 za mwaka 2022/23.
“Jumla ya tani 41,271.07 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 134,572 wenye thamani ya Shilingi bilioni 515.78 waliuzwa nje ya nchi na kuingizia Taifa mrabaha wa Shs. bilioni 14.44 ikilinganishwa na tani 29,466.98 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 150,308, wenye thamani ya Shs. bilioni 453.80, waliouzwa nje ya nchi na kuingizia Taifa mrabaha wa Shs. bilioni 12.56 katika mwaka 2022/2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 40.05 la mazao ya uvuvi yanayouzwa nje ya nchi,” akasema Ulega.
Ni wazi kwamba, vipaumbele vya mwaka huu vikitekelezwa vinaweza kuwa na matokeo chanya kwa asilimia kubwa kuliko mwaka uliotangulia, huku pia kukiwa na uhakika wa kutengeneza fursa za ajira kwa Watanzania.
Hili linadhihirishwa pia na Benki ya Dunia, ambayo katika Ripoti yake iliyozinduliwa Jumatatu, Juni 24, 2024, ilisema kwamba, mazingira yaliyopo nchini Tanzania yanatoa fursa kubwa ya kuongezeka kwa uzalishaji mifugo na kutengeneza fursa za ajira.
Licha ya kwamba kuna changamoto mbalimbali zikiwemo za hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi, lakini ripoti hiyo inasema, mazingira mazuri yaliyowekwa yanaweza kuwa chachu ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mifugo, huku ikisema kwamba, hata mahitaji ya mazao ya mifugo kama vile nyama, maziwa na mayai, yameongezeka kwa kiasi kikubwa.