Viongozi wapatiwe Takwimu sahihi – NBS

Na Sarah Moses, Dodoma

WATAKWIMU wa halmashauri, Wizara, idara, taasisi za umma wametakiwa kuwapatia viongozi wao takwimu sahihi zilizopata kibali kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu (NBS) wanapowasilisha taarifa zao kwa wananchi au viongozi wa juu ili kuepuka upotoshaji takwimu.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa, aliyasema hayo jijini Dodoma jana katika maadhimisho ya 33 ya kilele cha siku ya Takwimu Afrika 2023.

Maadhimisho hayo yameandaliwa na Ofisi ya Takwimu Tanzania (NBS) kwa kushirikiana na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika. 

“Watakwimu tufanye kazi ya ziada kuwapatia viongozi wetu takwimu sahihi, haipendezi kuona kiongozi akitoa takwimu ambazo sio sahihi kwa wananchi,” alisema.

Alieleza kuwa, watakwimu wanapaswa kuhakikisha takwimu wanazowapatia viongozi wao ziwe zimepata baraka kutoka NBS kwani ofisi hiyo ndiyo inayotoa takwimu sahihi zinazotumika sehemu yoyote. 

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotoa takwimu bora duniani ambapo umuhimu wa takwimu kwa nchi za Afrika unaendelea kuboresha uchumi kwa wananchi.

Alisema Tanzania inatoa takwimu bora zinazoaminika Afrika, duniani ambapo mwaka 2010, Serikali ilitekeleza mradi wa mpango kabambe wa takwimu hadi mwaka 2018 ulioimarisha upatikanaji takwimu bora nchini. 

“Nitoe wito kwa Ofisi ya Mtakwimu, sambazeni taarifa katika halmashauri zetu, takwimu zinapaswa kutumiwa kwa kutafsiri mipango ya maendeleo katika sekta zote.

“Pia takwimu zinasaidia nchi za Afrika kufahamu idadi ya rasilimali watu iliyopo na makundi yake,” aliongeza.

Kamisaa wa Sensa kutoka Zanzibar, Balozi Mohamed Ally Hamza, alisema lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu matumizi ya sense ambapo ushirikishwaji wa jamii unasaidia kuongeza thamani ya takwimu zetu.  

Maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika hufanyika Novemba 21 kila mwaka yakiwa na lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya takwimu katika mipango ya nchi za Afrika kwani takwimu zinahitajika wakati wowote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *