Viongozi wa dini msichoke kuwaunganisha watu – Biteko

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko, amewataka viongozi wa dini kutochoka kuunganisha watu ili kujenga Taifa lenye umoja, amani na mshikamano.
Dkt Biteko aliyasema hayo kwenye Mkutano wa Baraza la Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste ukiwa na lengo la kuombea amani, umoja miongoni mwa makanisa hayo.
Alisema Serikali inathamini mchango mkubwa unatolewa na viongozi wa dini nchini na kutoa wito kwa Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste kuunga mkono jitihada za serikali kuhakikisha amani inadumishwa.
 “Nawapongeza sana Baraza la Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste kwa kuwa na umoja na waumini wengi nchini wanaofikia milioni 12,” alisema.

Awali Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania-CPCT, Askofu Dkt Barnabas Mtokambali, alisema viongozi wa dini wanathamini jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha demokrasa, utawala bora na amani inadumishwa hapa nchini
“Tunaipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya kuhakikisha nchi iko kwenye utulivu, ustawi, amani na kuahidi kutoa ushirikiano, kuiombea Serikali,” alisema.
Mkutano huo ulianzishwa miaka thelathini iliyopita, kanisa hilo lina waumini milioni 12, tayari madhehebu 28 yako mbioni kujiunga na umoja huo wenye wanachama 128.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mwenyekiti wa kwanza wa Umoja huo, Askofu Dkt. Sylvester Gamanywa, Makamu Mwenyekiti wa CPCT, Askofu Dkt. Daniel Awet na Maaskofu kutoka Madhehebu mbalimbali chini ya umoja huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *