Mwalimu kutoka Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (Veta) mkoani Songea, Andrew Shayo amebuni mfumo wa usalama katika gari ambao ikiwa mlango wowote uko wazi basi haitawaka.
Ubunifu huo umefanyika ili kuondokana na ile tabia ya baadhi ya watu ambao huwasha gari kabla ya kufunga milango jambo ambalo ni hatari.
Mfumo huo ambao ameupa jina la Auto Electrical model pia huutumia katika kufundishia wanafunzi wa fani ya umeme wa magari katika chuo chake.
Akizungumza katika maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Shayo amesema lengo la kufanya ubunifu huo ni kutaka kuepusha athari zinazoweza kutokea ikiwa gati itawashwa kabla ya milango kufungwa.
“Tumezoea kuona kwenye gari kama mlango haujafungwa kuna sehemu inaonyesha kuwa kuna mlango uko wazi lakini katika mfumo huu gari haitawaka kabisa hivyo kumlazimu dereva kuhakikisha milango yote imefungwa ipasavyo kabla ya kuondoka, hii pia inamuambia kabisa ni mlango namba ngapi,” amesema Andrew.
Mbali na gari kugoma kuwaka kama milango haijafungwa vizuri pia huzima pindi mlango unapofunguliwa ikiwa ni ishara kwamba si salama.
“Lakini pia mfumo huu unaweza kutumiwa na mabasi makubwa kujua ni abiria gani hajafunga mkanda, ikiwa mtu hajafunga mkanda dereva anapewa ishara na kuambiwa ni siti namba ngapi ambayo mkanda haujafungwa hivyo ufuatiliaji unaweza kuwa rahisi kwa madereva,” amesema Shayo.
Katika upande wa kudhibiti wizi wa magari kwa kutumia funguo halisi, pia ameweka mlio ambao pindi funguo itakapochomekwa ili kuwasha gari kama si muhusika itapiga kelele.
“Hii ni kwa wale ambao magari huibwa na watoto au wezi tu, na pindi mlio huu utakapolia hautaweza kukoma hata kama funguo itachomolewa hadi pale mhusika atakapokuja kuzima switch iliyokuwa imewashwa kwa ajili ya usalama,” amesema Shayo na kuongeza:
“Katika hili tunakuwa tunahakikisha usalama zaidi, kwani itakulazimu kufunga mlango na kuuwekea lock ili kuhakikisha hakuna lolote baya linaweza kukupata maana siku hizi kumekuwa na tabia ya udokozi kwa watu waliokuwa kwenye magari, milango yao katika foleni inafunguliwa na kuibiwa.