Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya Samia Supa Cup ya Kata ya Msasani, yameanza kwa kishindo huku Diwani wa Kata hiyo, Luca Neghest akimwaga vifaa vya michezo kwa timu mbalimbali.
Mashindano hayo yamezinduliwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Kinondoni, Shaweji Abdalla Mkumbula kwa kushirikiana na viongozi wengine mbalimbali pamoja na Katibu Mwenezi wa CCM Dar es Salaam, Ally Bananga, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Msasani, Nyerere Mnyupe na Diwani Kata ya Tandale, Abdallah “Chief” Saidi.
Uzinduzi huo umepambwa na maandamano maalum yaliyowashirikisha wakazi mbalimbali, pikipiki aina ya bajaji ambayo yaliongozwa na Diwani Neghest.
Mkumbula amesema mashindano ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendeleza michezo nchini ambapo hadi sasa Tanzania imefikia viwango vya juu kabisa.

Amesema kila mwanamichezo anajua jinsi gani Rais Samia alivyochangia maendeleo ya michezo hadi sasa na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi nyota zinazotamba katika michezo barani Afrika.
“Kwa timu yetu ya Taifa ‘Taifa Stars’, kwa sasa tumefanikiwa kuingia mara mbili fainali za Afcon na mwaka 2027, sisi tutakuwa mwenyeji. Sisi kama wasaidizi wake, ni jukumu kumsaidia kwa kupitia Ilani ya CCM. Nampongeza Diwani Luca Neghest kwa kuandaa mashindano haya kwa kushirikisha soka, rede, bao na drafti kwa Kata ya Msasani,” amesema Mkumbula.
Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa Dar es Salaam, Ally Bananga, amempongeza Diwani Neghest kwa kuendelea kutimiza Ilani ya CCM na kuwaomba wakazi wa Kata hiyo kuendelea kumpa sapoti katika juhudi hizo.
Bananga amesema Diwani Neghest ameunga mkono juhudi za Rais Samia kwa kuandaa mashindano hayo yenye hamasa ya hali ya juu na tija kwa taifa.

“Kila mtu anajua kwa Rais Samia amesapoti Ndondo Cup, wachezaji wengi wa Tanzania wanatokea huku kwenye mashindano kama haya kwani yanaibua vipaji. Wito wangu kwa wadau ni kumpa sapoti kubwa Diwani Neghest na kuboresha viwanja vya michezo ikiwa pamoja na huu wa Msasani,” amesema Bananga.
Pia Mwenyekiti wa CCM wa Msasani, Nyerere Mnyupe, amewapongeza wanamichezo mbalimbali waliojitokeza kuunga mkono juhudi za Diwani Neghest za kutelekeza Ilani ya CCM kwa kuandaa mashindano ya aina mbalimbali yenye tija huku Diwani Kata ya Tandale,Abdallah Saidi akisema atatumia mashindano hayo kusaka vipaji kwa ajili ya timu ya KMC.
Kwa upande wake, Diwani Neghest amesema amefurahishwa na idadi na hamasa kubwa ya wakazi wa kata ya Msasani na sehemu nyingine kushiriki katika uzinduzi rasmi wa mashindanohayo.
“Nimefurahi sana kuona lengo la kuunga mkono juhudi za kuendeleza michezo kupitia Ilani ya CCM kutimia. Idadi ya watu na hamasa imenipa faraja sana. Nawashukuru viongozi wa CCM mliofika kunipa sapoti katika tukio hili lenye kutimiza ilani ya chama chetu kwa agizo la Rais Samia,” amesema Neghest.

Diwani Neghest amesema bingwa wa mashindano hayo atazawadiwa fedha taslimu sh, milioni 4 ambapo mbali ya soka, pia kiasi kama hicho cha fedha watazawadiwa washindi wa rede kwa wanawake na washindi wa pili watazawadiwa sh. milioni 2 kila mmoja.
Neghest amesema mshindi wa kwanza kwa mchezo wa drafti atazawadiwa sh. milioni 2 wakati mshindi wa pili atazawadiwa sh. milioni 1. Kwa upande wa bao, Neghesti amesema mshindi atapata sh. milioni 1 na mshindi wa pili atazawadisha sh. 500, 000.
Katika uzinduzi huo, timu ya Juventus FC iliifunga Don Bosco mabao 2-1.