Na Sarah Moses, Dodoma.
MKUU wa Mkoa wa Simiyu Anamringi Macha amesema uzalishaji wa Pamba hai katika Mkoa wa Simiyu umeongezeka kutoka Tani 10,300 mwaka 2021/2022 hadi Tani 12,285 mwaka 2022/2023, jambo lililopelekea Tanzania kuingia katika ramani ya uzalishaji duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Julai 18, 2025 Jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita amesema kuwa kuwa Tanzania ilishika nafasi ya saba na ya Tano katika uzalishaji wa Pamba hai ikitanguliwa na Nchi za China, India, Uturuki na Tagekistani.
Amesema kuwa asilimia 80 ya Wananchi wa Mkoa wa Simiyu wanategemea Kilimo, katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 Mkoa uliendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha Sekta hiyo na kupata mafanikio makubwa.
Aidha katika hatua nyingine ameongeza kuwa, jumla ya Shilingi Bilioni 89.34 zimepokelewa kwa ajili kutekeleza miundombinu ya kuboresha huduma ya Maji, ambapo Shilingi Bilioni 63.73 zimetumika kutekeleza Miradi 85 ya Maji vijijini.
Lakini pia Shilingi Bilioni 25.61 zimetumika kutekeleza Miradi 61 katika miji ya Bariadi, Maswa, Busega na Meatu ambayo yote imekamilika na inatoa huduma.
“Upatikanaji wa huduma ya Maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 60.85% mwaka 2020 hadi asilimia 71.0 mwaka 2025, aidha, kwa upande wa upatikanaji wa maji mjini umeongezeka kutoka asilimia 60.5 mwaka 2020 hadi asilimia 75.7 mwaka 2025. Hivyo upatikanaji wa Maji katika Mkoa ni 73%,” amesema.
Katika hatua nyingine amesema kuwa Mkoa huo umeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uanzishwaji wa Viwanda ambapo katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa viwanda kutoka 671 mwaka 2020 hadi 1,342 mwaka 2025 kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji.
“Viwanda vikubwa kutoka vinane mwaka 2020 hadi 15 mwaka 2025, viwanda vya Kati kutoka vinne mwaka 2020 hadi 10 mwaka 2025, Viwanda Vidogo kutoka 660 mwaka 2020 hadi 1,317 mwaka 2025, Viwanda vikubwa na vya kati vinahusika na uchakataji wa Pamba, Chaki na Mafuta ya Alizeti na Pamba, kutengeneza bidhaa za Plasitki,”amesema.
Mwisho.