Uzalishaji asali Mbinga wapaa kwa asilimia 5.1

Na Stephano Mango, Mbinga

UZALISHAJI wa asali katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga umeongezeka kwa asilimia 5.1 mwaka 2022/23 ikilinganishwa na mwaka 2021/22.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Amina Seif, Afisa Nyuki wa Halmashauri hiyo Gilbert Gotifrid alisema kuwa katika kipindi tajwa tani za asali zilizovunwa ziliongezeka kutoka 3.9 hadi 4.1.

Gotifrid alisema kuwa ongezeko hilo limechagizwa na kuongezeka kwa mwamko wa wananchi katika shughuli za ufugaji wa nyuki.

Alisema kuwa nwamko umekuwa ukiongezeka siku hadi siku ingawa bado si wakuridhisha sana ikilinganishwa na ukubwa wa maeneo ya ufugaji tuliyonayo

Gotifrid alisema mwaka 2022/23 wafugaji nyuki ambao ni watu binafsi na taasisi waliongezeka kufikia 84 ikilinganishwa na 42 za mwaka wa nyuma yake.

Kwa upande mwingine, vikundi vilivyokuwa vinajihusisha na ufugaji wa nyuki viliongezeka kutoka 32 hadi kufikia 40, ingawa bado fursa za ufugaji nyuki hazijatumiwa ipasavyo.

“Kati ya hekta 900 zilizopo katika milima ya Lipembe ambazo zimetengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji wa nyuki, ni kama asilimia 1.1 tu zinatumika kwa shughuli hiyo,” alisema. 

Alieleza kwamba ili kutumia vizuri fursa zilizopo kitengo chake kimekuwa kikitoa elimu kuhusu ufugaji wa nyuki kupitia vipeperushi pamoja na redio zilizopo katika halmashauri.

Gotifrid alisema kuwa asali inawasaidia wafugaji wa nyuki kujipatia pesa na kuongeza kipato chao na kwa pande wa afya, asali inafanya uwiano mzuri wa sukari mwilini pia inawasaidia watu wenye vidonda vya tumbo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *