Na Mwandishi Wetu, Dodoma
RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, ameshauri fedha zinazotengwa katika bajeti ya serikali zitumike vizuri ili kuleta tija.
Dkt. Kikwete aliyasema hayo jana jijini Dodoma katika mkutano wan ne wa maendeleo ya biashara na uchumi.
Hivi karibuni uliibuka mjadala uliohusu ubadhirifu wa fedha za umma uliobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mjadala huo ulitikisa bungeni jijini Dodoma ambapo baadhi ya wabunge walishauri wabadhirifu wanyongwe.
“Hakikisheni mnatumia vizuri pesa kidogo mnazopata maana kilichojitokeza, wakati mwingine tunalalamika kuhusu bajeti lakini hata fedha kidogo tulizopewa, matumizi yake siyo mazuri,” alisema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kikwete alisema ili uchumi wa nchi yoyote ukue, serikali inapaswa kuboresha mazingira ya uwekezaji.
“Uwekezaji unastawi pale ambapo mazingira yake yanakuwa rafiki,” alieleza.
Akizungumzia kongamano hilo, aliwashauri washiriki wake kulitumia ili kupata ushirikiano wa kufanya tafiti na kuleta majawabu ya matatizo yanayoikabili jamii.
“Kongamano kama hili linaleta fursa, kuibua mtazamo na mbinu mpya za kutatua changamoto zinazoikabili jamii,” alisema Dkt. Kikwete.
Aliongeza kuwa, Rais anapoingia madarakani hawezi kujua kila kitu ndiyo maana anakuwa na washauri wake pamoja na wasaidizi kama Mawaziri, Makatibu Wakuu wanaompa ushauri.
“Unapoingia unakuwa hujui kila kitu na ukiwa Rais unatakiwa kushughulika na kila jambo hivyo lazima uwategemee washauri wako.
“Ndio maana Rais ana Mawaziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu, Makamishna na Wakurugenzi, pale Ikulu ana ofisi binafsi yenye mabingwa wa kumshauri,” aliongeza Dkt. Kikwete.