Na Bwanku M Bwanku.
Bandari ni eneo lililobeba uchumi mkubwa sana. Zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa na huduma zote zinazoingia nchini kutoka Nje ya Nchi zinapitia bandarini. Wengi wanaliita lango kuu la uchumi wa nchi.
Tanzania imepata bahati ya kuwa kwenye ukanda wa kimkakati (strategic location) kwa kuzungukwa na mataifa 6 yasiyokuwa na bandari (landlocked countries) ambayo yanategemea bandari zetu hasa bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo yao kutoka nje. Mataifa hayo ni kama Zambia, Kongo, Uganda, Malawi, Rwanda na Burundi.
Fursa hii kubwa ya kijiografia inafanya Tanzania kuwa na fursa nyingi sana kwenye eneo la bandari hasa ikiwekezwa vyema na kuvutia sehemu kubwa ya mizigo yote inayoingia ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika jambo litakalofanya Taifa kuvuna mapato na fedha nyingi mara mbili zaidi ya tunazopata sasa kwenye eneo hili.
Wataalamu wengi wa uchumi wanasema bado kama Taifa hatujanufaika vya kutosha kimapato ukilinganisha eneo la kimkakati la kijiografia la Taifa letu na mataifa mengi yanayotumia bandari zetu.
Bandari ni eneo lililobeba uchumi mkubwa sana. Kama tukiwekeza vyema, nusu ya bajeti yetu itatoka bandarini. Lakini ni muhimu Watanzania kuelewa kwamba, meli na mizigo inapochelewa kupakua mizigo bandarini ina athari moja kwa moja na bei ya bidhaa mtaani maana bandari ikiwa na ufanisi mdogo na hivyo meli na mizigo kuchelewa kutoka bandarini Wafanyabiashara wanalipa ushuru na hapo tegemea bei ya bidhaa kupanda.
Licha ya Taifa letu kuwa na bandari muhimu katika eneo la kimkakati kijiografia hasa kuzungukwa na mataifa mengi yasiyokuwa na bandari yanayotumia bandari yetu, bado hatupati mapato mengi zaidi bandarini kwa kinachofahamika wazi ufanisi mdogo wa bandari zetu kuhudumia meli na shehena za mizigo kwa haraka.
Kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto nyingi bandarini ikiwemo kuchelewa kupakuliwa mizigo, meli kuchukua muda mrefu kupakua mizigo na aina zingine za usumbufu zinazoleta kero kubwa kwa Wafanyabiashara na watumiaji wengine wa bandari, jambo linalosababisha baadhi wengine kukwepa kutumia bandari yetu na kupitishia mizigo yao kwenye bandari jirani ya Beira ya Msumbiji na ile ya Mombasa nchini Kenya.
Leo ukimuuliza mfanyabiashara anayetumia bandari ya Dar es Salaam atathibitisha uchelewaji mkubwa wa kutoa mzigo bandarini pamoja na meli kuchukua muda mrefu kupakua mizigo kunakosababishwa na ufanisi mdogo wa bandari na miundombinu duni. Meli zinachukua zaidi ya siku 5 na upakuaji mizigo wakati katika bandari za wenzetu shughuli kama hizo zikichukua muda mfupi usiozidi hata siku mbili.
Changamoto hii ya ufanisi mdogo wa bandari zetu umesababisha baadhi ya wafanyabiashara kukimbilia kutumia bandari zingine kama ya Mombasa na Beira kwasababu ya urasimu na uchelewaji wa hapa kwetu na hivyo Taifa kukosa mapato mengi sana yatokanayo na bandari. Na ndipo tunaposema licha ya kuwa kwenye eneo la kimkakati kijiografia bado hutujafaidi vya kutosha na bandari, mapato yako chini licha ya kwamba uwekezaji mkubwa ukifanywa mapato yataongezeka mara mbili yasasa.
Msululu huu wa changamoto za bandari nchini unaofanya tukose mapato mengi na kwa dhamira ya Serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutaka kufungua uchumi zaidi ili tupate uwekezaji mkubwa utakaoleta uchumi na maendeleo makubwa, ndipo ukafungua ukurasa mpya wa kuwekeza zaidi bandarini ili tupate faida nyingi zaidi ya tunazopata sasa, tuongeze mapato, tuharakishe utoaji na upakuaji mizigo, tufaidi eneo la kimkakati la kijiografia ilipo bandari yetu na kufanya maboresho makubwa ya bandari.
Ndipo ukurasa mpya wa kufanya uwekezaji mkubwa bandarini na kampuni kubwa ya DP World yenye uzoefu mkubwa inavyofanya kazi na mataifa zaidi ya 50 duniani kote, ikiwemo Afrika.
Baada ya changamoto hizi nyingi zinazopunguza ufanisi wa bandari yetu na kutukosesha mapato mengi, Serikali ya Rais Samia kupitia kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ikaamua kutafuta wawekezaji wenye uzoefu mkubwa kwenye sekta ya bandari na ndipo ikaanza majadiliano ya kutafuta wawekezaji wapya hatimaye kupatikana DP World na kisha makubaliano na kampuni hiyo ya Dubai ya DP World kwa lengo la kuanzisha ushirikiano katika uendelezaji na uwekezaji wa maeneo ya bandari nchini.
Kampuni ya DP World ni moja ya makampuni yenye uzoefu mkubwa sana wa zaidi ya miaka 10 kwenye biashara ya bandari duniani. Ni kampuni inayomilikiwa na Serikali ya Falme za Kiarabu (UAE) ikiwa na uzoefu mkubwa wa kuongeza mapato na ufanisi wa bandari ambapo mpaka sasa kampuni hii inafanya kazi katika mataifa zaidi ya 50 duniani kote.
Marekani anaendesha bandari zao zaidi ya 1, Uingereza (2), Canada, China, Ujerumani, Ufaransa huku hapa Afrika ikiwekeza kwenye bandari kwenye nchi zaidi ya 10 ikiwemo Nigeria, Rwanda, Msumbiji, Misri, Afrika Kusini na nyingine.
Kampuni ya DP World imekuwa ikifanya vizuri duniani kote kwa kuongeza mapato na ufanisi mkubwa zaidi wa uendeshaji wa bandari ikiwa na teknolojia ya kisasa kufanya shughuli hii hasa kwa kuzingatia uendeshaji wa bandari unahitaji teknolojia kubwa na ya kisasa itakayowezesha uharaka na ufanisi mkubwa. Mataifa yote inakofanya kazi imeongeza mapato makubwa na kuongeza mizigo na meli kwa kutumia mtandao wake mkubwa ulionao kwenye sekta ya bandari.
DP World ikiwekeza Tanzania tutaongeza mara mbili mapato, kupunguza sana muda wa meli na mizigo kukaa bandarini na hivyo kupunguza gharama bandarini na moja kwa moja kushusha bei ya bidhaa mtaani kwa wananchi kwani mara nyingi bidhaa zimekuwa zikipanda kwasababu ya kuchelewa kwa mizigo kutoka bandarini kunakotozwa ushuru na kusababisha wafanyabiashara kuongeza bei bidhaa.
Baada ya Jumamosi Juni 10, 2023 Bunge kupitisha rasmi azimio la Serikali kutaka kuingia mkataba na kampuni hiyo ya Dubai, sasa Taifa linaelekea kwenye uwekezaji huu mkubwa wa bandari zetu na kampuni ya DP World.
Makubaliano haya na DP World ya kuboresha bandari nchini yakianza na mkataba kuanza kutekelezwa na kazi kuanza, italeta mapinduzi makubwa sana nchini kwenye sekta ya bandari na kushusha uchumi na maendeleo makubwa kwa Taifa.
Manufaa yatakayopatikana kupitia mkataba wa Serikali ya Tanzania na Kampuni ya DP World ya nchini Dubai ni pamoja na kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 kwa sasa mpaka masaa 24. Hii itapunguza gharama za utumiaji wa bandari yetu. Hii itarudisha wafanyabiashara wengi waliokimbia kutumia bandari yetu kwasababu ya kuchelewa kwa upakuaji mizigo.
Kuongeza idadi ya meli zitazokuja bandari ya Dar es Salaam kutoka meli 1,569 zilizohudumiwa mwaka 2021/22 mpaka kufikia takribani meli 2,950 ifikapo mwaka 2032/33.
Kupunguza muda wa ushushaji wa makontena kutoka siku 4.5 mpaka siku 2, kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka masaa 12 mpaka saa 1 kutokana na uboreshaji Wa mifumo yạ TEHAMA.
Kupunguza gharama ya usafirishaji wa shehena kutoka nchi za nje kwenda nchi za jirani, kwa mfano kutoka Dola za Marekani 12,000 mpaka kati ya Dola 6,000 hadi 7,000 kwa kasha linalokwenda nchi ya
Malawi, Zambia au DRC. Hii italeta watumiaji wengi kwenye bandari ya Dar es Salaam ikiwemo kurudisha wale waliokimbia kwasababu ya gharama kubwa ya utumiaji wa bandari yetu unaotokana na ufanisi mdogo.
Kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22 hadi kufikia tani 47.57 mwaka 2032/33 sawa na ongezeko la asilimia 158.
Maboresho haya makubwa moja kwa moja yataongeza mapato ya Serikali yatokanayo na kodi ya forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa bandarini kutoka Shilingi Trilioni 7.76 za mwaka 2021/22 hadi Shilingi Trilioni 26.70 za mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 244.
Ajira pia zitaongezeka zinazotokana na shughuli za bandari kutoka 28,990 mwaka 2021/22 hadi 71,907 ifikapo mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 148.
Maboresho ya magati ya kuhudumia majahazi na abiria ikiwa ni pamoja na kushawishi uingiaji wa meli kubwa za kitalii zitakazoongeza idadi ya watalii nchini na kuongeza pato la Taifa.
Mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika bandari zote (knowledge and skills transfer) kutoka katika uzoefu wa kampuni hii ya DP World.
Uanzishaji wa maeneo huru ya kiuchumi na kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi ikiwemo sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, utali, viwanda na biashara.
Kuchagiza ukuaji wa sekta zingine za usafirishaji kwa njia ya reli (SGR, TAZARA na MGR) ambazo sasa zitapata mzigo mkubwa wa kusafirisha kwasababu ya meli nyingi zinazoingia bandarini.
Kampuni ya DP World ina uzoefu mkubwa kwenye bandari na itaongeza mara mbili ya mapato na kuondoa changamoto za muda mrefu za bandari yetu zinazotuchelewesha.
Bwanku M Bwanku.