
Na Mwandishi Wetu, Dar es Saalam
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, leo ametumia zaidi ya saa mbili kuzungumza na kumtembeza mtoto mwenye kipaji kutoka Dodoma kwenye maeneo aliyotamani kuyaona jijini Dar es Salaam.
Wiki hii, picha mjongeo za mtoto huyo, Ridhiwani Asheri, mwenye umri wa miaka 13, zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikiionyesha uwezo wake mkubwa wa kubuni ujenzi wa barabara na madaraja akiwa kijijini kwao Kibaigwa, Dodoma.
Baada ya Ulega kuona picha hizo, aliagiza wataalamu wa wizara yake kwenda kumwona na kuangalia namna ya kumsaidia.
Baada ya kumwona na kuzungumza na familia, Waziri aliomba mkutano nao ili kuangalia namna bora ambayo serikali inaweza kufanikisha ndoto zake.
Baada ya mkutano wa jana katika ofisi ndogo za Wizara ya Ujenzi jijini Dar es Salaam, Ulega alisema serikali ya Tanzania ina historia, uwezo na dhamira ya kusaidia watoto wenye uwezo mkubwa kimaarifa kwa maslahi ya Taifa.
Baada ya mazungumzo hayo Waziri Ulega, aliahidi kumsaidia kijana huyo kuhakikisha anatimiza ndoto zake za kuwa Mhandisi mkubwa hapo baadaye.
Waziri Ulega alisema atakaa na Wizara ya Elimu kuona ni sehemu gani sahihi kijana huyo apelekwe ili kuweza kumsaidia kielimu hasa kwenye masuala ya ujenzi.
Pia Waziri Ulega alimtembeza mtoto huyo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ili kujionea kwa macho yale ambayo alikuwa anayatengeneza akiwa nyumbani kwao kwa kuyaona tu kwenye TV.
Miongoni mwa maeneo hayo ni Daraja la Kijazi lililopo Ubungo, Daraja la Tanzanite na kituo cha Treni ya Mwendokasi (SGR) Posta.



