Na Mwandishi Wetu, Lindi
UJENZI wa vyoo bora na upatikanaji wa maji ya uhakika katika Shule ya Msingi Mahumbika iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama mkoani Lindi, umepunguza utoro kwa wanafunzi na kuwafanya wasome kwa utulivu.
Mwenyekiti Kamati ya Shule ya Msingi Mahumbika, Selemani Omary Ndomondo, anasema shule hiyo imekuwa na uhaba wa vyoo kwa muda mrefu ambapo wanafunzi walilazimika kufuata maji nyumbani na wanaoishi jirani na shule walilazimika kwenda nyumbani kujisaidia ili kuepuka foleni kubwa iliyokuwepo hasa wakati wa mapumziko.
Licha ya shule hiyo kuwa kongwe lakini ilikuwa na matundu nane tu ya vyoo yaliyokuwa yakitumiwa na watoto 500, ambapo shule hiyo ilikuwa inahitaji ukarabati wa mkubwa siyo kwa vyoo tu, bali hata madarasa ambayo yamechakaa.
Ndomondo anasema: “Kwa sasa tuna matundu tisa ambayo tulitengenezewa na mradi wa maji na vyoo unaotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la Heart to Heart Foundation kwa udhamini wa shirika la HANA Foundation kutoka nchini Korea Kusini.
“Baada ya kukamilisha wanafunzi wote walihamia kwenye vyoo vipya hali ambayo ilimshawisi mfadhili kuboresha vyoo nane vya awali vilivyokuwepo shuleni, hivyo kuanza kutumika pia.”
Ramadhani Bakari, mmoja wa wanafunzi wa shule ya Msingi Mahumbika, anasema kuwa wengi walikuwa wakikimbilia nyumbani kwenda kujisaidia kutokana na foleni kubwa iliyokuwepo shuleni hapo hasa nyakati za mapumziko.
“Lakini tulikuwa tunachelewa baadhi ya vipindi darasani, hii kwetu ilikuwa haitupi utulivu wa akili kabisa, lakini kwa sasa kuwepo kwa matundu ya kutosha shuleni ya vyoo yanatupa utulivu wa akili.
“Hebu fikiri wanafunzi zaidi ya 500 tulikuwa tunatumia matundu sita pekee, sasa wavulana tunayo nane na wasichana wanayo tisa, hii kwetu ni moja kati ya mafaniko makubwa sana,” anasema.
Salumu Musaa, mwanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Mahumbika, anasema ili wapate maji ya kutumia shuleni walikuwa wanalazimika kwenda bondeni kuchota, maana bila maji hawawezi kunywa, kunawa na kwenda chooni, jambo lililokuwa changamoto kubwa kwao.
“Tulikuwa tunakwenda bondeni kuchota maji, wanafunzi wengine walikuwa wanatoroka wanakwenda majumbani kujisaidia na wakirudi wanakuta kipindi kimekaribia kwisha, lakini sasa tumepata maji na vyoo ambavyo tunaamini vimetupa nafasi ya kufurahi, wakati mwingine tunakwenda tu chooni kuangalia picha walizochora,” anasema.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mahumbika Beno Kiyeyeu, anaeleza namna wanafunzi wa shule hiyo walivyonufaika na mradi wa vyoo na maji katika shule hiyo ambayo kwa muda mrefu imekuwa na changamoto.
“Wanafunzi zaidi ya 500 walikuwa wakitumia matundu sita pekee, kwa sasa angalau tumepata matundu nane kwa wavulana na matundu tisa kwa wasichana ambayo yatapunguza changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa,” anasema.
Somoe Ally Kanduru, mzazi na mkazi wa Mahumbika, anasema wanafunzi wengi walipata magonjwa yatokanayo na kinyesi yaani kuhara na mengine yatokanayo na maji kwa kiasi kikubwa.
Mradi huu wa maji ni mradi umeongeza usafi shuleni hata watoto wetu tunawaona wakiwa wasafi wenye utulivu wa aakili hta ndoo zetu sasa zimepumzika majumbani maana walikuwa wakipoteza kila siku na tunalazimika kuwpaa zingine ili waweze kwenda na maji shuleni.
“Huu mradi siyo kwamba umewafaa wanafunzi, hata sisi wanakijiji tunaoishi jirani na eneo hili tumenufaika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa sasa tunapata maji eneo la karibu na tunaamani maji ya uhakika yapo, tulikuwa tukifuata maji mbali,” alisema Kanduru.
Ofisa wa Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira kutoka shirika lisilo la kiserikali la Heart to Heart Foundation, Estoni Waliha, anasema waliona uhaba wa vyoo katika shule hiyo na hakukuwa na uwiano kati ya wanafunzi na idadi ya matundu ya vyoo yaliyokuwepo shuleni hapo.
“Tumetengeneza vyoo bora vizuri ambavyo siyo tu mtoto atajisaidia katika mazingira bora, lakini hata elimu tumetoa ya unawaji kwa njia ya picha, hii itamuwezesha mtoto kujua mengi na kulinda afya yake.
“Tunaamini kuwa tukiungana kulinda afya za watoto wetu tunaweza kufanikiwa kwa kuwa na maji na vyoo bora shuleni na majumbani pia.
“Sasa hakuna tatizo, wanafunzi walihamia vyoo vipya kutokana na uzuri wa vyoo tukalazimika kukaa chini na mfadhili ili kumuweka sawa na kuzungumza naye ambapo alikubali kufanya maboresho katika matundu nane ya awali ili angalau yafanane na haya mapya, hivyo tumekamilisha.
“Shule nyingi za msingi zinahitaji msaada wa maji na pia vyoo bora, wanaosoma katika shule hizo ni watoto ambao wanahitaji kupewa msingi bora wa elimu sahihi,” anasema Waliha.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama wakati wa kukabidhiana mradi huo, Dkt. Dismas Masulubu, anasema kuwa mradi huo umeokoa watoto wengi na kusaidia jamii katika masuala ya vyoo na maji kwenye jamii, shule na huduma za afya katika zahanati na vituo mbalimbali vya afya.
“Yaani huu mradi umetunufaisha kwa kiasi kikubwa, jamii yetu inapaswa kupata elimu kwa vitendo ili iweze kubadilika na kuepukana na magonjwa yatokanayo na kinyesi sambamba na upatikanaji wa maji ya ukakika shuleni na kwenye vituo vya afya ambayo yameweza kuwasaidia wanajamii wanaoishi jirani na huduma hizo.
“Mradi huu umezinufaisha shule 20 kwa kujenga matundu ya vyoo bora na kuweka vyoo vya watu wenye ulemavu pamoja na chumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kubadailisha nguo wanapokuwa kwenye hedhi, lakini pia zaidi ya vituo vya afya 10 vimepatiwa huduma mbalimbali zikiwemo huduma za maji ya uhakika,” anasema Dkt. Masulubu.