Uingizaji wa vibali vya kemikali waongezeka kwa asilimia 294

Na Sarah Moses, Dodoma.

KATIKA miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita kumekuwa na ongezeko la vibali vya uingizaji wa kemikali kutoka vibali 40,270 kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 hadi vibali 158,820 kufikia Desemba, 2024 ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 294 ya vibali vilivyotolewa. 

Hayo ameyasema Machi 14,2025 jijini Dodoma Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita .

Amesema Mamlaka hiyo imeweka mazingira mazuri ya uingizaji na usafirishaji wa kemikali hatarishi na zile zinazodhibitiwa chini ya mikataba ya kimataifa ili kulinda afya ya binadamu, mazingira na usalama wa nchi kwa kutoa vibali vya kuingiza na kusafirisha kemikali hizo. 

“Pamoja na uwepo wa mazingira mazuri, kasi ya utoaji vibali imeongezeka kutokana na wadau kuongeza uelewa wa Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayosimamia shughuli za kemikali pamoja na kuwajengea wadau uelewa wa matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA inayotumika katika uombaji wa usajili na vibali. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 294 ya vibali vilivyotolewa”, amesema.

Amesema  uchunguzi wa Kisayansi wa kimaabara kwa sampuli/vielelezo umeongezeka kutoka sampuli 155,817 Mwaka Fedha 2021/2022 hadi kufikia sampuli 188,362 kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 21.

 Katika kipindi cha mwaka wa Fedha huu wa 2024/2025, kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2024, sampuli 108,851 zilifanyiwa uchunguzi sawa na 

asilimia 104.50 ya lengo la kuchunguza sampuli 104,161. 

Ongezeko la sampuli zinazochunguzwa na Mkemia Mkuu wa Serikali linatokana na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi na wadau wa Mamlaka na ubora wa huduma za uchunguzi zitolewazo na Mamlaka. 

Aidha, ongezeko hili ni kutokana na ushirikiano na taasisi za serikali za udhibiti kama vile Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulenya (DCEA), Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato (TRA), na wadau wa afya zikiwemo hospitali, OSHA na NEMC na wadau wengine wanaotumia huduma za Mamlaka ili kupata uhakika wa ubora wa bidhaa zao 

Pia amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, GCLA imeendelea kuchangia uboreshaji wa mazingira ya biashara ya kemikali nchini hasa zile za kimkakati zinazotumika kwenye uchimbaji na uchenjuaji wa madini hapa nchini na nchi jirani ambapo kemikali aina ya Ammonium Nitrate imeongezeka kutoka tani 135,445 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi tani 359,629.56 kufikia Desemba, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 165.52.

“Vile vile, kemikali ya Salfa imeongezeka kutoka tani 396,982 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi tani 1,136,214.86 kufikia Desemba, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 186.21 huku kemikali ya Sodium Cyanide  imeongezeka kutoka tani 41,461 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi tani 53,055.9 kufikia Desemba, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 27.97” amesema.

Ametaja sababu za kuongezeka kwa uingizaji wa kemikali hizo kupitia Bandari ya Dar es Salaam na Tanga kuwa ni pamoja na maboresho ya miundombinu ya bandari pamoja na mahusiano mazuri yaliyowekwa na Serikali kati ya nchi na nchi jirani.

Mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *