Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
UAMUZI wa kesi inayowakabili wabunge 19 wa Viti Maalum (CHADEMA) akiwemo Halima Mdee na wenzake utatolewa Desemba 14, 2023.
Uamuzi huo umetolewa jana na Jaji anayesikiliza kesi hiyo kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Cyprian Mkeha wakati kesi hiyo ilipoitwa ili iweze kupangiwa tarehe ya hukumu.
Mdee na wenzake walifukuzwa uanachama na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wabunge hao walifunga usikilizwaji wa kesi Septemba 7, 2023 baada ya kumaliza kuwahoji wajumbe sita wa Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA.
Mdee aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (BAWACHA) na wenzake 18 walifungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu.
Wabunge hao walikuwa wakipinga kufukuzwa uanachama kwa utaratibu wa mapitio ya mahakama ambapo jopo la mawakili wao liliwaita mahakamani Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini CHADEMA.
Mawakili hao ni Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashu. Lengo la kuwaita ni kuwahoji kuhusu uhalali wa utaratibu uliotumika kuwavua uanachama wabunge hao.
Hata hivyo, jana Jaji Mkeha alisema kesi hiyo iliitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama pande zote zimekamilisha kuwasilisha hoja na kasha kupanga tarehe rasmi ya uamuzi.
Alisema kwa kuwa pande zote zimewasilisha hoja zao, mahakama itatoa hukumu Desemba 14, 2023.
Katika kesi hiyo, Mdee na wenzake wanapinga uamuzi wa Baraza Kuu la CHADEMA kutupilia mbali rufaa zao wakipinga uamuzi ya Kamati Kuu kuwafuta uanachama wakituhumiwa kuapishwa kuwa wabunge bila ridhaa ya chama hicho.
Kamati Kuu iliwavua uanachama wa chama hicho Novemba 27,2020 hivyo walikata rufaa Baraza Kuu wakipinga uamuzi wa Kamati Kuu.
Katika uamuzi wake wa Mei 11, 2021, Baraza Kuu lilitupilia mbali rufaa yao, Mdee na wenzake walikimbilia mahakamani na kuomba kibali cha kufungua shauri hilo.
Mdee na wenzake wanapinga uamuzi wa Baraza Kuu wakidai pamoja na mambo mengine, hawakupewa haki ya kusikilizwa ambayo ni ya msingi.
Wanaiomba mahakama itengue mchakato na uamuzi huo, kuiamuru CHADEMA itemize wajibu wake wa kisheria kwa maana ya kuwapa haki ya kusikilizwa, kutoa zuio kwa Spika na NEC kuchukuliwa hatua yoyote hadi malalamiko yao yatakapoamuriwa.
Mbali ya Mdee, wabunge wengine ni Ester Matiko, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Cecilia Pareso, Hawa Mwaifunga, Ester Bulaya na Grace Tendega.