Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Kwa ujibu wa taarifa hiyo, watu 10 wanahusika na mtandao wa uhamishaji fedha kinyume cha taratibu.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo jana ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma, Majaliwa alisema watumishi wote wa umma lzima atunze, kuratibu vizuri matumizi ya fedha zinazopatikana.
“Taarifa nimeipokea na mapendekezo na kamati, hatua za haraka zichukuliwe kwa sababu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatafuta fedha za kuleta maendeleo lakini kuna watu wachache wanafanya ubadhirifu,” alisema.
Aliwataka Mawaziri na Makatibu Wakuu wasiridhishwe na taarifa za miradi wanazopokea pindi wakiwa ziarani, wataalamu wanatoa taarifa nzuri mbele ya viongozi hao lakini bado kuna mipango waliyoifanya.
Akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Kigoma, Septemba 20-22, 2023, Majaliwa alipata taarifa ya uwepo wa fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ya Amana ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kutoka TAMISEMI.
Fedha hizo ziliondolewa baada ya muda bila maelekezo maalum wala kujua zilitumikaje.
“Hapa Manispaa mnapokea fedha, zinakaa kwenye akaunti kwa muda halafu zinapotea, hazijulikani zimefanya nini. Nitaleta timu, waje wafuatilie hapa Kigoma, waende hadi TAMISEMI ili tuone huo mnyororo unaenda wapi,” alisema Majaliwa.
Majaliwa alikuwa akizungumza na viongozi wa dini, Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenye Ukumbi wa NSSF.
Awali akitoa taarifa kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa timu ya uchunguzi, Shedrack Kimaro, alisema timu hiyo ilibaini kuwa uchepushaji fedha hizo unafanyika kwa kutumia njia kadhaa ikiwemo kuomba kibali kutoka HAZINA cha kuvuka na bakaa ya fedha za miradi mwaka wa fedha unapokaribia kwisha.
“Timu ya uchunguzi imebaini sh. milioni 463.59 zilitumwa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na hazikuwa kwenye mpango wala bajeti ya Manispaa na hazijawahi kuombewa matumizi kama bajeti ya ziada,” alisema.
Aliwataja watumishi waliohusika na uchepushaji wa fedha hizo ni Ferdinand Filimbi, Salum Juma Said, Kombe Kabichi, Athumani Msabila, Moses Zahuye.
Wengine ni Jema Mbilinyi, Mhandisi Joel Shirima, Aidan Mponzi, Tumsifu Kachira na Mzee Ubwa.
Alisema watumishi hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Alongeza kuwa, mbali ya watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma, wamo pia maafisa kutoka TAMISEMI, HAZINA na baadhi ya wafanyabiashara ambao wanatumiwa ili kupitisha miamala ya fedha hizo.
Wakati huohuo, Mwenyekiti huyo alisema kuna ubadhirifu mkubwa unafanyika kupitia Kitengo cha Usimamizi wa Fedha katika Akaunti Jumuifu ya Amana kilichopo TAMISEMI.
“Timu imebaini kuwa Kitengo cha Usimamizi wa Fedha katika Akaunti Jumuifu ya Amana kilichopo TAMISEMI kinahusika kutuma fedha kwenye halmashauri mbalimbali na kisha kuzitoa kwa kushirikiana na watumishi wa halmashauri hizo,” alisema.
Alisema baadhi ya halmashauri zinakuwa hazijaomba kibali cha kuvuka na fedha za bakaa kutoka HAZINA lakini zinatumiwa fedha hizo.
“Kuna halmashauri ambazo zinaomba kibali lakini zinapewa pungufu ya fedha zilizoomba na zinazobakia hazijulikani zinafanya nini,” aliongeza.