Na Mwandishi Wetu
KIKUNDI cha Umoja wa Kinama cha Tuliponga Kikoba, kimesaidia Kituo cha Watoto Yatima cha Nyota Njema kilichopo Bomba mbili kwa Kapungu Kata ya Msongola, Dar es Salaam.
Tuliponga Kikoba kilianza rasmi umoja huo Januari 21, mwaka huu kikiwa na jumla ya wanachama 30.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Mhasibu wa kikundi hicho, Tandi Sam Sikalngwe, amesema wamejipanga kuwa na kikoba bora ambacho kitaleta manufaa katika jamii.
Amesema licha ya kuwa kikoba hicho bado kichanga lakini wamefanikiwa kuwasadia watoto yatima na wasiojiweza kwa kuwapelekea mahitaji mbalimbali ili wawezi kujikimu.
Kiongozi huyo amesema Tuliponga kitakuwa kikoba cha aina yake na kinavyozidi kukua watu wengi watafaidika.
“Kwanza tunashukuru kwa umoja wetu tumeweza kukubaliana na kuwatembelea watoto yatima, hawa ni watoto wetu na ujio wetu ni faraja kubwa kwao,” amesema Tandi na kuendelea.
“Kikubwa ambacho tumefanya ni kuandaa chakula cha jioni ambacho tumejumuika kula nao pamoja, lakini pia vifaa vya shule, sukari, unga, mchele na baadhi vitu vingine, ilikuwa faraja kubwa kwetu na kwa watoto”.
Aidha ameongeza mpango wao thabiti ni kuhakikisha Tuliponga Kikoba kinasajiliwa haraka na tayari wameshaanza hatua za awali.
“Unapoamua kufanya jambo zuri lazima ulipange katika msingi bora, tumeshaanza hatua za awali za usajili, lengo kuwa na kikoba ambacho kinafahamika na kufanya harakati zake vizuri,” amesisitiza Mhasibu huyo.
Hata hivyo kiongozi huyo alisema Nyota Njema ndio kituo cha kwanza kutembelea lakini wamejipanga kutembelea vituo vingi sehemu mbalimbali jijini Dar es salaam.