Na Zahoro Mlanzi
BAADA ya Klabu za Simba na Azam FC, kuwapima afya baadhi ya wachezaji wake kabla ya kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2023/24, Bodi ya ligi hiyo (TPLB), imesema mchezaji yeyote ambaye hatapima afya hatoruhusiwa kucheza ligi hiyo msimu huo.
Klabu hizo kwa nyakati tofauti zilianza zoezi hilo jijini Dar es Salaam, kitu ambacho kinaleta afya kwa afya za wachezaji soka nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TPLB chini ya Ofisa Habari, Karim Boimanda, klabu zote za ligi hiyo, Championship na First League zinapaswa kuwafanyia vipimo vya afya wachezaji wao.
“Wachezaji wote waliopangwa kutumika kwa msimu wa 2023/24 wanapaswa kupimwa afya zao ili kutekeleza takwa la kikanuni na masharti ya leseni za klabu,” alisema Boimanda.
Alisema wachezaji hao lazima wathibitishwe na daktari kuwa hawana matatizo yoyote yanayoweza kuhatarisha usalama wao na wachezaji wengine.
“Wachezaji hawatofanyiwa vipimo vya afya na kupata cheti cha utimamu wa afya, watakosa sifa za kusajiliwa na kupatiwa leseni maalum za usajili wa wachezaji zinazotolewa na TFF, hivyo hatoruhusiwa kucheza mashindano yoyote yaliyo chini ya shirikisho hilo,” alisema Boimanda.
Alisisitiza zoezi hilo ni muhimu na lazima kwa mujibu wa Kanuni ya 69:2(2.4) ya Ligi Kuu na Ligi ya Championship pamoja na Kanuni ya 70:2(2.4) ya First League kuhusu maombi ya usajili, hivyo klabu zote zinapaswa kuhakikisha wanafanya hivyo chini ya daktari mwenye sifa na vigezo vinavyohitajika.