TPA kujenga matanki yao ya mafuta

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), inakusudia kujenga matanki yake kwa ajili ya kuhifadhi nishati ya mafuta ili kuondoa ucheleweshaji wa meli za mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Meneja wa Kituo cha kupakulia mafuta, Mhandisi Yona Malago (pichani), aliyasema hayo jana wakati akitoa ufafanuzi kwa wanahabari waliotembelea bandari hiyo.
Alisema tayari Mkandarasi wa ujenzi wa matanki hayo ameshapatika baada ya serikali kutenga kiasi cha fedha katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2023/2024.
“Kwa sasa serikali haina matanki ya kuhifadhi mafuta, tunategemea matanki ya watu binafsi hivyo tukijenga matanki yetu tutaondokana na hali ya ucheleweshaji wa meli za mafuta bandarini,” alisema Malago.
Naye Abasi Msukulu, alisema meli kubwa za mafuta yanayoingizwa nchini huchukua kati ya siku tatu hadi nane kushusha kulingana na wapokeaji wa mafuta wanavyopokea.

Msukulu aliwaeleza wanahabari waliotembelea boya maalumu la kushusha mafuta ya dizeli lililopo eneo la Kisinda Mji Mwema.

Alisema uwekezaji uliofanywa na serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, umesaidia meli kubwa za mafuta zaidi ya tani 50,000 hadi 100,000 kushushwa katika boya hilo lililopo kwenye kina kirefu cha maji ya Bahari ya Hindi.

Katika hatua nyingine, maboresho yanayoendelea kufanyika katika Bandari hiyo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa malalamiko ya wananchi hasa wizi wa baadhi ya vifaa vya magari katika bandari hiyo ambayo inatumiwa na nchi mbalimbali za Ukanda wa Afrika.

Afisa Utekelezaji Msaidizi Bandari ya Dar es salaam, Aman Kimario, aliyasema hayo kwenye ziara ya wanahabari waliofika kujionea maboresho hayo.

Alisema kwa sasa magari zaidi ya 1,500 yanapakuliwa kutoka katika meli saa nane kwa siku kutokana na uboreshaji wa kuongeza gati maalumu namba ziro kwa ajili ya magari.

“Kwenye gati namba ziro ambayo ina eneo lake maalumu, zaidi ya magari 3,000 yanapaki kwa wakati mmoja jambo ambalo limesaidia kuboresha utendaji kazi.

“Kama mteja atakamilisha taratibu zote za forodha anaweza kuondoka na gari yake ndani ya siku moja” alisema Kimario.

Kwa mujibu wa Kimario, udokozi wa vifaa vya magari kwa sasa haupo kutokana na mifumo mizuri waliyoiweka, kuongeza kamera katika eneo la gati namba ziro.

“Kwa sasa ukisikia kuna gari vifaa vyake havionekani jua kabisa gari hilo vifaa hivyo vimepotea huko lilipotoka na sio hapa kwenye Bandari ya Dar es salaam,” aliongeza.

Wakati huo huo, zaidi ya tani 1,500 za mizigo mchanganyiko hupakuliwa kwa siku kutoka katika meli mbalimbali zinazotia nanga katika bandari hiyo.

Afisa Mwandamizi Kitengo cha Mizigo Mchanganyiko, Juma Juma aliyasema hayo wakati akitoa ufafanuzi kwa wanahabari waliotembelea bandari hiyo.

Alisema hali ya hewa ikiwa mbaya kwa maana ya kuwepo mvua husababisha changamoto ya ushushaji  mizigo mchanganyiko, kusababisha mizigo kuchukua muda mrefu kupakuliwa kutoka kwenye meli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *