TOMA yazindua mpango mkakati wa miaka mitano

Na Tatu Mohamed, Dar es Salaam

TAASISI ya Tanzania Online Media Alliance (TOMA) imezindua Mpango Mkakati wa miaka mitano ijayo kuanzia mwaka 2024 hadi 2028.

Akizindua Mpango huo jana Novemba 22, 2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC), Kenneth Simbaya, amewataka viongozi kuwa na nidhamu ili kuweza kufikia malengo.

“Mipango mikakati mingi inafeli kwasababu ya kutokuisimamia vizuri… ushauri wangu msisahau malengo yenu kwani safari ndio kwanza mmeianza. Fanyeni kazi kwa bidii, pambaneni ukilinganisha na mazingira ya ushindani katika soko mnalokwenda kulifanyia kazi.

“Lazima tuhakikishe mpango mkakati unaendana na miundombinu iliyopo ili kuleta maendeleo. Hata hivyo mambo yote haya yanahitaji nidhamu,” amesema na kuongeza:

“Hata barabara tunazopita usipofuata kanuni unapata ajali na mpango mkakati utekelezaji wake unahitajika nidhamu ya kazi. Hakikisheni TOMA inawaunganisha pamoja waandishi wa habari za mtandaoni.”

Pia ameshawauri kuhakikisha TOMA inatumia uwapo wa mitandao kwa manufaa ya umma.

“Mitandao ina mambo mengi, ina faida na hasara. Sasa TOMA lazima mhakikishe mnaitumia kwa manufaa ya umma…hiyo itaongeza kuaminika,” amesema.

Akiizungumzia TOMA, Makamu Mwenyekiti, Salome Kitomari, amesema inaundwa na wanahabari zaidi ya 200 wanaopandisha maudhui mtandaoni nchi nzima.

“Tumeandaa mpango mkakati huu kwa kusaidiwa na Freedom House, tunawashukuru kwa msaada huo mkubwa kuhakikisha waandishi wa habari mtandaoni mnatuleta pamoja. Ndani ya mpango mkakati huu tutahakikisha mambo yote yapo ikiwamo kuwawezesha wanahabari kuendana na teknolojia,” amesema Kitomari. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *