Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba Nchini (TMDA), inaendesha mafunzo ya siku tatu Jijini Dar es Salaam ya kufanya tathmini ya udhibiti wa vifaa tiba vya Wamama, Watoto wachanga na Watoto kwa wataalam wa vifaa tiba kutoka Mamlaka za Udhibiti za nchi 11 za Afrika.
Kongamano hilo ni la kwanza Barani Afrika ambalo mafunzo hayo yanafanyika kufuatia nchi za Afrika kutokuwa na uwezo wa kudhibiti bidhaa hizo, hivyo mafunzo hayo yatasaidia uwezo wa kutathimini bidhaa kabla hazijaingia kwenye soko.
Kongamano hilo la siku tatu, limezinduliwa mapema na Mkurugenzi wa Vifaa Tiba na Vitendanishi, Kissa Mwamwitwa, aliyekuwa amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, ambapo aliipongeza serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Afya kwa kuipa uwezo TMDA kujulikana Afrika na kuweza kutoa utaalamu ambao wanatoa kwa nchi zingine.
“Warsha hii imedhaminiwa na wadau wa maendeleo USAID-MTaPS, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Jukwaa la Afrika la Udhibiti wa Vifaa tiba, AUDA-NEPAD na TMDA.
“Tunaishukuru serikali ya Tanzania kupitia Rais wetu Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Afya kwa kutupatia uwezo ambao tunaonekana Bara la Afrika,’’ amesema Kissa Mwamwitwa. Amesema watabadilishana uzoefu ili kupata watalaam watakaokuwa wana uwezo wa kusaidia eneo hilo la vifaa tiba kwa akinamama na watoto kabla havijaingia sokoni.
“Ili kundi lilikuwa nyuma la akina mama, watoto wachanga na watoto wadogo. Hivyo kupitia mafunzo haya wadhibiti watakuwa wanatumika katika kutoa utalaam katika nchi zao baada ya kujifunza.
Mafunzo hayo yalifanyika kutokana na kuwa na upungufu upande huo na ni mara ya kwanza kufanyika barani Afrika na tunashukuru Tanzania kuwa mwenyeji na pamoja na uwenyeji pia tumetoa watalaama ambao watashiriki kutoa mafunzo,’’ Amesema Kissa Mwamwitwa.
Wataalam hao wanatoka katika Mamlaka za Udibiti wa Vifaa Tiba na Vitendanishi kwa nchi za Afrika ikiwamo Uganda, Kenya, Ethiopia, Nigeria, Afrika Kusini, Botswana, Zambia, Rwanda, Ghana, Senegali na mwenyeji Tanzania.