
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imeendelea kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya dawa na vitenganishi ndani ya maonesho ya 49 ya Kimataifa ya biashara (SabaSaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Temeke, Dar Es Salaam.
Akizungumza katika Banda la Stone town ndani ya maonesho hayo ya Sabasaba, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, amesema kama mamlaka mara kwa mara wataendelea kutoa elimu kwa umma ili kusaidia jamii kuwa na uelewa wa matumizi sahihi ya dawa.
Amesema majukumu makubwa ya TMDA ni kusajili dawa za ndani na zinazotoka nje kuingia nchini hii ni pamoja na kufanya ukaguzi kila siku ikiwamo kwenye maduka ya Dawa, masoko na mipaka ili kumlinda mtanzania.
“Sisi jukumu letu kuhakikisha kwamba dawa inatumika kama ilivyokusudiwa na sio kumdhuru mtumiaji. Majukumu yetu ni kuhakikisha tunasajili dawa zilizosajiliwa na kukidhi soko la nchi, yote hii ni kumlinda Mtanzania katika usalama wa dawa hivyo tunahakika ubora na ufanisi.
Vile vile tunafanya kazi tunapima bidhaa za dawa kupitia Maabara zetu za kisasa ambazo zina ubora wa Kimataifa wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO)”. amesema Dkt. Fimbo.
Aidha, katika banda hilo la TMDA, Dkt. imbo ametoa elimu kwa wananchi waliotembelea juu ya matumizi sahihi ya dawa na kuacha kutumia bidhaa hiyo kiholela bila kufuata maelekezo na ushauri wa wataalamu ili kuepuka usugu wa dawa.

