Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeundwa kisheria kuhakikisha inalinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za dawa za binadamu na mifugo, vifaa tiba na vitendanishi.
TMDA ambayo ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya, Kati ya majukumu hayo, moja kubwa ni kufanya kaguzi za mara kwa mara za dawa na vifaa tiba katika kanda na maeneo yote zinakopatikana huduma hizo nchini.
Chini ya Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo kwa kushirikiana na watendaji wake, wanatekeleza shughuli mbalimbali za kimamlaka katika kuhakikisha jamii inakuwa salama, lakini inakuwa na uelewa wa kile wanachotekeleza.
Lengo ni kuendelea kushirikiana na jamii katika kufichua taarifa za uhalifu na kufichua bidhaa za bandia katika kuhakikisha usalama wao pamoja na mifugo.
Katika Makala haya, mwandishi anaangazia namna mamlaka hii inavyopiga hatua za kiutendaji katika kutimiza wajibu wao na kusukuma mbele maendeleo katika kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza azma ya kuhudumia Watanzania wote kwa usawa na uwiano kupitia mamlaka hii.
INAVYODHIBITI UBORA
TMDA Kupitia Kanda ya Mashariki, kuanzia Desemba 12 hadi 24, mwaka jana, ilifanya ukaguzi wa dawa na vifaa tiba katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia na kubaini asilimia 62 ya maduka ya dawa muhimu hayana watoa huduma wenye sifa.
Kupitia ukaguzi huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mafia, Kassim Ndumbo, anachukua hatua za haraka kwa kuagiza maduka hayo yafungwe.
Anaagiza kuendelea kufanyika kwa ukaguzi mara kwa mara ili kuchukua hatua kwa watoa huduma na wafanyabiashara wanaokiuka sheria, kanuni na maadili yanayohusika na utoaji wa huduma za afya.
Naye Mkaguzi wa TMDA, Japhari Said, anasema katika zoezi hilo, walikagua jumla ya majengo 50 ikiwa ni vituo vya kutolea huduma za afya 24 na maduka ya dawa muhimu 26.
“Maduka 16 hayakuwa na wahudumu wenye sifa, 14 yamebainika kuuza dawa zisizo ruhusiwa kuwapo kwenye maduka ya dawa muhimu.
“Lakini pia tumebaini maduka tisa hayakuwa na kibali chochote, tisa mengine yakiwa na dawa zilizo kwisha muda wa matumizi zikiwa hazijatengwa moja likiuza dawa za serikali,” anasema Saidi.
YAKAMATA WAHALIFU
Katika kutekeleza jukumu kudhubiti ubora, TMDA Kanda ya Mashariki Aprili 14, mwaka huu, inafanya ukaguzi na kufanikiwa kumkamata mhalifu mwenye kiwanda bubu cha kutengeneza dawa bandia.
Kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, TMDA inafanikiwa kumkamata anayetengeneza na kusambaza dawa za binadamu bandia, mkazi wa Kipawa, Ilala, Williams Mwangile (39).
Mtuhumiwa huyo ambaye alikutwa nyumbani kwake anakutwa na vielelezo vinavyoonesha kufanya uhalifu huo ambavyo dawa, lebo na vifungashio.
Mtuhumiwa huyo ambaye inadaiwa hutengeneza na kusambaza dawa hizo mijini na vijijini na nchi jirani, anakamatwa kufuatia uchunguzi wa TMDA na vyanzo mbalimbali vya kipelelezi kubaini na kumfuatilia mtuhumiwa huyo.
Mkaguzi wa Dawa wa TMDA Kanda ya Mashariki, Japhari Mtoro, anasema; “TMDA ilikuwa inamtafuta mtuhumiwa huyu Williams, mkazi wa Matembele Lodge eneo la Kipawa Ilala Dar es Salaam, kwa tuhuma za kuzalisha na kusambaza dawa hizo bandia, kwa mfumo wa makopo kinyume cha kifungu cha 76 cha sheria ya dawa na vifaa tiba sura ya 219.”
Anaeleza kuwa, baadhi ya washirika wake, walishakamatwa na TMDA na baadhi ya dawa hivyo alikuwa bado yeye peke yake.
“Nyumbani kwake tumebahatika kupata lebo 537 ambazo zina majina ya dawa mbalimbali, (printed labels) Lakini pia tulikuta makopo 12 tupu ambayo pia yanatumika kufungasha dawa,
“Pia tulikuta viroba vitatu, kiroba kimoja unga wa njano na viwili unga mweupe.” anasema Japhari
Hata hivyo baada ya kukamilika upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa, usiku wa manane walipekua nyumbani kwa wazazi wake ambapo walibaini uwapo wa vitu mbalimbali ikiwamo vifungashio vitupu ya dawa aina ya rangi mbili ‘capsule’
“Lakini pia nako tumekuta lebo, jumla ya lebo 142 Nyumbani kwa wazazi wake, ambao inafanya jumla ya lebo zilizokamatwa kuwa 679, kwa hiyo baada ya kumpata mtuhumiwa huyu ataunganishwa na wale waliokamatwa kwa ajiri ya kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria,
Anasema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya atakayethibitika kujihusisha na uzalishaji na usambazaji wa dawa bandia,
“Lakini pia nitumie fursa hii kuwashukuru sana wadau mbalimbali na viongozi wa serikali ya mtaa, jeshi la Polisi, wananchi kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyu, kwani tulikuwa tunamtafuta tangu mwezi wa Tatu mwaka huu, hadi leo tumemkamata,” anasema Japhari.
UDHIBITI BIDHAA ZA TUMBAKU
Mbali na kukamata bidhaa hizi, ifahamike TMDA pia jukumu la kudhibiti matumizi ya bidhaa za tumbaku nchini.
Jukumu hilo limekasimishwa kwa TMDA tangu Aprili 30, 2021 kupitia Tangazo la Serikali Na. 360.
Kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku, Sura 121 kimetafsiri maeneo ya umma kama mahali ambapo haparuhusiwi kuvuta sigara ni zinakotolewa huduma ya afya, maktaba, mahali pa ibada, majengo au maeneo yaliyotengwa kwaajili ya mikutano ya kitamaduni na kijamii, shughuli za michezo au burudani.
Mengine sehemu za huduma ya chakula, majengo ya ofisi, vyombo vya usafiri wa anga, ardhi au maji, mabanda ya maonesho, masoko, maduka makubwa na maeneo mengine yoyote yanayotumiwa na umma.
Kwa mujibu wa Dkt. Fimbo, kifungu cha 13 cha sheria tajwa kimeruhusu uvutaji kwenye baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na taasisi za elimu ya juu, majengo ya ofisi, hoteli, baa, migahawa na maeneo ya burudani ambayo yanapaswa kutenganisha vyumba au maeneo maalum ya kuvutia na kutovutia tumbaku.
YAWANOA WATENDAJI WAKE
Katika kutekeleza majukumu yake pia TMDA inawanoa watumishi wa kada ya afya ambao wanahusika na kufanya ukaguzi wa dawa na vifaa tiba nchini katika kuboresha ufanisi wao ili kulinda afya za watumiaji wa dawa na vifaa tiba.
Meneja wa TMDA, Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa, akiwa kwenye mkutano wa kuwanoa watumishi wa kada hiyo, anasema lengo ni kuwaongezea ujuzi wakaguzi ili kufanya kazi ya ukaguzi kwa kuzingatia sheria.
Mkumbwa anasema kuwa wakaguzi watatekeleza kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo kama zilivyotolewa na TMDA kama vile kufanya ukaguzi wa maeneo yanayohusika na utunzaji, uuzaji na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, kufanya ufuatiliaji na kutoa taarifa za ubora na usalama wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika soko.
Anaongeza kuwa, wakaguzi watatakiwa kuchukua sampuli za bidhaa zinazodhibitiwa kwaajili ya uchunguzi wa kimaabara pale inapohitajika na kufanya ufuatiliaji wa madhara/matukio yanayohisiwa kusababishwa na matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Mkumbwa anasema kuwa wakaguzi wanatakiwa kufanya uhakiki wa bidhaa zisizofaa kwa matumizi kabla ya uteketezaji kwa kujaza fomu ya uhakiki (Kiambatisho Na.7) baada ya mawasiliano na Ofisi ya Kanda ya TMDA na kusimamia zoezi la kuteketeza bidhaa ambazo hazifai kwa matumizi baada ya uhakiki na kisha kujaza fomu ya uteketezaji (Kiambatisho Na. 8) na kuiwasilisha ofisi ya Kanda ya TMDA kwaajili ya kuandaa cheti.
Anaenda mbali naa kuagiza kila halmashauri kuandaa na kuwasilisha taarifa za utendaji kazi kwenye Ofisi za TMDA za Kanda na kuwasilisha nakala kwa Katibu Tawala wa Mkoa ambazo ni taarifa ya utendaji ya robo mwaka na taarifa ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi za udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa katika soko.
Aidha, TMDA inakutana na wadau wa dawa kujadili kwa kina changamoto zinazohusiana na usajili wa dawa.
Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Wanyama kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA),Yona Mwalwisi, anasema wanategemea kupata maoni ya wadau ili waweze kuboresha huduma.
“Tumekutanisha wadau wa famasi, hospitali ambao ni watumiaji wa dawa tunategemea na kupata maoni ya vifaa tiba pia ni mkutano muhimu kwa mamlaka, kwani tutapokea maoni ambayo yatasaidia kuboresha mifumo yetu ya usajili, uingizaji na usafirishaji wa dawa nje ya nchi,”anasisitiza.
Umuhimu wa warsha hiyo katika kutoa mrejesho kwa wadau wao kwa sehemu ambazo hawajaenda vizuri, kwasababu kuna vitu wanatakiwa watekeleze, hivyo mkutano unatoa nafasi kwa pande zote mbili namna ya kuboresha huduma.
“Suala la dawa na vifaa tiba walengwa ni wagonjwa kama mamlaka tunataka kuhakikisha mgonjwa ambaye anatumia bidhaa hizo apate bidhaa bora, salama na fanisi lengo ni kuendelea kumlinda Mtanzania,”anaeleza.
Mwalwisi anasema watatumia nafasi hiyo kuwaelimisha sheria na taratibu za dawa ili wawalinde wananchi.
“Kwenye upande wa uingizaji kikubwa ni kuzingatia sheria na taratibu za uingizaji kulingana na vigezo tunavyohitaji,” anasema.
YAGUSA SEKTA YA HABARI
TMDA pia imeenda mbali kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari kwa kuamini jukumu lao la kutoa elimu kwa jamii bila wanahabari, kunaipa ugumu utekelezaji wa kazi hiyo.
Ndio sababu ikaanzisha tuzo maalumu kwa kazi za Waandishi wa Habari juu ya Udhibiti wa Dawa, Vifaa tiba, Vitenganishi na bidhaa za tumbaku kwa mwaka 2021-2022.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMDA, tuzo hizo ni kwa Waandishi wa Habari ambao wameripoti taarifa na kuandaa makala mbalimbali kuhusu kazi na majukumu ya TMDA katika kipindi cha kuanzia Juni 2021hadi Februari mwaka huu.
Mwaka jana ilitoa tuzo na zawadi kwa wanahabari waliofanya vyema katika ushindani wa kazi walizowasilisha TMDA.
Aidha, imebainisha kuwa, kazi zinazolengwa ni zile zilizoripotiwa kupitia Televisheni (TV), Redio, Magazeti na mitandao ya Kijamii kipindi hicho cha Juni 2021 hadi Februari mwaka huu.
KUSAIDIA JAMII DAWA, VIFAA TIBA
Mbali na kutoa huduma, TMDA inaona umuhimu wa kuwa na jukumu la kusaidia jamii ambapo kwa Kanda ya Mashariki inakabidhi msaada wa dawa za binadamu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia zenye thamani ya zaidi ya milioni 6 kwa lengo la kusaidia matibabu ya wananchi wasiyo na uwezo.
Mkaguzi wa Dawa, Japhari Saidi kwaniaba ya Meneja wa TMDA Kanda ya Mashariki, Adonis Bitegeko, anasema lengo ni kusaidia wananchi wenye uwezo mdogo au wasio na uwezo kabisa kuchangia gharama za matibabu ili nao wapate dawa zenye ubora, usalama na ufanisi uliothibitishwa na TMDA.
“Dawa hizi zinatokana na sampuli zilizobaki baada ya uchunguzi wa kimaabara kukamilika na kufaulu vipimo.Hivyo, Ndugu Mkurugenzi naomba uzipokee ili ziweze kutumika kusaidia matibabu ya wananchi wa Mafia,”anasema Saidi.
HATI SAFI
Pamoja na kutekeleza majumu makubwa ya kiutendaji TMDA imeendelea kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa katika kuzitumia fedha fedha inazopewa na serikali.
Katika kuthibitisha hilo TMDA inakabidhiwa hati safi ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2021/22.
Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, akikabidhi hati safi hiyo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba-TMDA, (MAB), Eric Shitindi, anaeleza kujivunia mafanikio hayo.
Anasema yote yanatokana na utekelezaji wa maelekezo na ushauri unaotolewa na Bodi unayoiongoza kwa lengo la kuepuka hoja mbalimbali za kiukaguzi.
“Nikiwa kama Mtendaji Mkuu wa kila siku pamoja na timu nzima ya Menejimenti,nikiri kuwa tunayo furaha na tunajivunia mafanikio haya ambayo yamekuwa ni rekodi nzuri kwa Taasisi na hata kwa Wizara mama,” anasema Fimbo.
Mwenyekiti wa Bodi Shitindi naye anaipongeza TMDA kwa kupata hati safi kwenye ukaguzi wa hesabu za mwaka wa Fedha 2021/22 na kuielekeza mamlaka kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa na mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za Serikali CAG ili kuendelea kupata hati safi.
“Sisi kama bodi tunapata faraja na fahari kusimamia taasisi ambayo inatambua na kutekeleza mifumo thabiti ya kiutendaji ikiwa ni pamoja na kusimamia ipasavyo rasilimali zilizopo kwa maslahi mapana na nchi,” amesema Shitindi.
TMDA, tangu kuanzishwa kwake, imeweka rekodi ya kupata hati safi kwa miaka takriban 15 mfululizo ambapo maelekezo na ushauri unaotolewa na CAG katika kila kaguzi yamekuwa yakizingatiwa.