TMA: Novemba-Januari kutakuwa na mvua nyingi

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema kipindi cha nusu ya msimu (Novemba, 2023-Januari, 2024) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ukilinganisha na nusu ya pili (Februari-Aprili 2024).

Hali hiyo inatokana na uwepo wa El-Niño unaotarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za msimu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, alisema mwelekeo wa mvua za msimu, maeneo ambayo yanapata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ni mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma, Singida na Dodoma.

Mingine ni Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Kusini mwa Morogoro.

“Mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo ya Kusini mwa Mkoa wa Morogoro, mikoa ya Iringa, Lindi, Mtwara, Singida, Dodoma, Kaskazini mwa Mkoa wa Katavi, Kigoma na Tabora.

“Aidha, mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa Kusini mwa Mkoa wa Katavi, mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya na Ruvuma,” alisema.

Chang’a ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia Nchi (IPCC), alisema athari zinazoweza kujitokeza ni vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi na mafuriko vinaweza kujitokeza.

Kutokana na kuzidi kwa unyevu, kutaathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, kina cha maji katika mito na mabwawa kikitarajiwa kuongezeka.

Aliwashauri wadau mbalimbali kuzingatia matumizi endelevu ya uhifadhi wa rasimali maji.

Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a alisema msimu wa vuli kwa miezi ya Oktoba-Desemba, 2023 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga.

Pia Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Pwani (Kisiwa cha Mafia) na Zanzibar (visiwa vya Unguja na Pemba) utabiri wake ulishatolewa.

Mvua hizo tayari zimeanza katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, Pwani ya Kaskazini na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki kama ilivyotabiriwa.

“Ongezeko la mvua linatarajiwa miezi ya Novemba- Desemba, 2023, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kunyesha Januari na Februari, 2024,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *