Timu ya wataalam SADC watembelea TMA

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaaam

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imepokea timu ya wataalamu kutoka Kituo cha Kikanda cha Huduma za Hali ya Hewa cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika “SADC Climate Service Centre- (SADC CSC) wanaoratibu utekelezaji wa mradi wa SADC wa kuboresha huduma za hali ya hewa kwa nchi wanachama wa “Intra-ACP Climate Services and related Applications (ClimSA)”.

Wataalamu hao wamefanya ziara hiyo Agosti 18, 2025 katika ofisi za TMA zilizopo Ubungo Plaza, Dar es Salaam wakiongozwa na msimamizi wa mradi huo, Surekha Ramessur.

Lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa ni kukagua utendaji kazi wa vifaa ambavyo vimetolewa msaada na kituo hicho cha “SADC CSC” kwa Tanzania kupitia TMA kupitia mradi wa SADC ClimSA na kuvikabidhi rasmi kwa TMA kwa matumizi ya kitaasisi.

Vifaa hivyo vilivyokaguliwa na kukabidhiwa kwa TMA ni pamoja na mtambo wa kuchakata data na kuandaa taarifa za tahadhari ya hali mbaya ya hewa, Kanzidata mbili na mtambo kuhifadhi data za hali ya hewa.

Makabidhiano rasmi ya vifaa hivyo yalifanyika ofisini kwa Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi, Dkt. Pascal Waniha, ambaye alipokea kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, ambapo alishukuru Sekretarieti ya SADC kwa kuendelea kuzisadia nchi wanachama kupitia program za kikanda za kuboresha huduma za hali ya hewa.

Kwa upande wake, kiongozi wa timu hiyo, Surekha Ramessur, alipongeza TMA kwa hatua kubwa iliyopiga katika utoaji wa huduma za hali ya hewa na kuahidi kwamba Kituo hicho kitaendelea kushirikana na TMA kupitia jitihada za kikanda za kuboresha huduma za hali ya hewa kwa nchi wanachama wa SADC.

Aidha, wataalamu hao walipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na TMA pamoja na kutembelea ujenzi wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Tsunami.

Mradi wa Intra CLimSA, unatekelezwa kwa nchi wanachama wa SADC Tanzania ikiwa mojawapo, chini ya ufadhili wa mfuko wa Maendeleo Nchi za Jumuia ya Ulaya (EDF).

Mradi huo unalenga kuimarisha zaidi uwezo wa nchi wanachama wa SADC katika utoaji wa huduma za hali ya hewa na utabiri wa hali ya hewa, hususani tahadhari za hali mbaya ya hewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *