TIA yatahadharisha wanafunzi wapya kuhusu uhusiano na walimu

Na Mwandishishi Wetu, Singida

WANAFUNZI wapya waliochaguliwa kujiunga na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida kwa msimu wa masomo wa 2023/24 wametakiwa kutojihusisha na uhusiano wa kimapenzi na walimu.

Kaimu Mkurugenzi wa Kampasi hiyo ambaye pia ni Mratibu wa Taaluma,  Flora Lemnge, ameyasema hayo juzi Oktoba 30, 2023 katika semina elekezi kwa wanafunzi hao na kueleza kuwa mwanafunzi atakayejihusisha na uhusiano  wa kimapenzi   kwa lengo la kujaziwa matokeo mazuri kwenye mitihani yake  atakuwa amejivua utu wake bure.

Akizungumzia namna ya usahihishaji wa mitihani hiyo, amesema ukusanywa na kusahihishwa sehemu moja na hakuna mwalimu anayesahihisha darasa alilofundisha anapangiwa darasa lingine.

Amesema kila swali husahihishwa na mwalimu mmoja  hivyo mtihani wenye maswali matano husahihishwa na walimu watano tofauti.

“Sasa hivi nasimama kama mama nafasi yangu ya kitaaluma naiacha kwa muda ‘ewe binti usivue nguo zako kisa upate mtihani itakula kwako’ kuna baadhi yenu mmekuja hapa na kuanza kujipangia walimu baada ya kuona anamshara na yupo ‘smati’ atakukula bure kwani mtihani huo ni uleule utashindanishwa na kampasi zingine za TIA na unasahihishwa na walimu wa ndani na wa nje na si vinginevyo,” amesema Lemnge.

Lemnge amewataka wanafunzi hao kuzingatia sheria zote za taasisi hiyo na nchi na kuhudhuria masomo kwasababu hilo ndilo jambo walilolikusudia wakizingatia kuwa wazazi wao wamekuwa wakitoa fedha nyingi kwaajili yao.

Amesema lengo la semina hiyo ni kuwafanya wazijue taratibu zote za taasisi hiyo ukizingatia kuwa wanafunzi hao wametoka katika mikoa mbalimbali na kuwa na tabia tofauti.

Naye Mshauri wa Wanafunzi katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Ambwene Kajula amewapongeza wanafunzi kwa kuchagua chuo hicho na akawashuru wazazi kwa jinsi wanavyojitoa kuwasomesha watoto wao.

Amesema baadhi ya mambo yanayofundishwa katika semina hiyo elekezi ni kutaka kuwaonesha wanafunzi hao mazingira watakayokuwa nayo na jinsi ya kuishi  na kufikia malengo waliyoyakusudia.

Aidha, Kajula amesema pia watawakutanisha na wadau kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) watu wa dawati la jinsia, Mfumo wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Taasisi za kifedha kama benki, vyombo vya mawasiliano ya simu na kuwafundisha mbinu mbalimbali za kimaendeleo.

Naye Mratibu wa Mipango na Dawati la Malalamiko wa taasisi hiyo, Magreth Emmanuel, amewataka wanafunzi hao wanapokuwa na changamoto mbalimbali kuziwasilisha kwa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho.

“Kunatabia baadhi ya wanafunzi wakipata changamoto wanazipeleka kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, TAKUKURU na maeneo mengine hiyo sio sahihi inatakiwa uanzie chini kwa viongozi wa serikali ya wanafunzi (TIASO) ambao wakishindwa kutatua tatizo lako wanatuletea sisi viongozi wa chuo,” amesema Emmanuel.

Rais wa Serikali ya wanafunzi (TIASO) wa chuo hicho, Godfrey Mbuya, amesema moja ya jukumu lao ni kutatua changamoto mbalimbali za wanafunzi na pale zinapowazidi uwezo wanazipeleka ngazi ya juu.

Mbuya amesema semina hiyo ni ya muhimu sana kwao kutokana na mwingiliano wa wanafunzi kutoka maeneo na makuzi tofauti ikiwa ni pamoja na kuyajua mazingira ya chuo na kufuata sheria kanuni na taratibu za chuo.

Mwanafunzi wa Shahada ya kwanza katika Rasilimali Watu na Utawala, akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake aliushukuru uongozi mzima wa taasisi hiyo kwa semina hiyo elekezi yenye lengo la kuwajenga na kupata miongozo mbalimbali na kuwa mambo yote waliyoelekezwa ni wajibu wao kuyatekeleza.

Maximilian ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwaongeza bumu na hela ya kujikimu kutoka Sh. 8,500 hadi Sh. 10,000 ni jambo la kuendelea kumshuru kwa kuwa anataka tuwe na Taifa la watu walioelimika.

Amesema baadhi ya mambo wanayotakiwa kuyafanya wakati wakiwa chuoni ni kuzingatia uvaaji wenye staha, utunzaji wa mazingira na vifaa vya chuo, heshima kwa kila mtu, lugha nzuri, kushiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo michezo na kutojihusisha na vitendo vya wizi na mapenzi ya jinsia moja (ushoga na usagaji)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *