TEA yampa kongole Samia ufadhili wa miradi ya elimu

  • Yatumia Shs. 30 bilioni utekelezaji wa miradi 2022 – 2023
  • Watanzania 49,060 wanufaika na mafunzo ya ujuzi

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA), imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuinua sekta ya elimu nchini, ambapo ndani ya kipindi cha miaka miwili mamlaka hiyo imeweza kutekeleza miradi mingi ya elimu kwa gharama ya zaidi ya Shs. 30 bilioni.

Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dkt. Erasmus Kipesha, amewaambia wahariri wa vyombo vya habari nchini kwamba, jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Rais Samia zimekuwa chachu kubwa ya ufanisi wa mamlaka hiyo katika kutekeleza miradi ya maendeleo ya elimu nchini.

“Tunaishukuru sana Serikali ya Rais Samia kwa jitihada hizi kubwa inazofanya katika kuhakikisha ubora wa elimu unaongezeka hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

“Tunaishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambayo sisi tuko chini yake kwa kuweka mazingira mzzuri ya kuhakikisha TEA inatekeleza majukumu yake, lakini tunaishukuru Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Fedha pamoja na wizara nyingine mtambuka,” alisema.

Akizungumza na wahariri hao jijini Dar es Salaam Novemba 20, 2023 katika mfululizo wa vikao kazi vinavyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa taasisi za umma kueleza mafanikio, majukumu na changamoto zao, Dkt. Kipesha alisema kwamba, kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa unaoratibiwa n TEA, ufadhili na utekelezaji wa miradi ya elimu kwa Bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023, jumla ya Shs. bilioni 10.99 ziligharimia ufadhili wa miradi 132 ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule 151 nchini.

Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa vyumba 114 vya madarasa katika Shule 38 zikiwemo Shule 2 za Sekondari na Shule 36 za Msingi.

Dkt. Kipesha alisema, mradi uonatarajiwa kunufaisha jumla ya wanafunzi 6,840, umegharimu kiasi cha Shs. 3,345,620,180.

Kati ya vyumba hivyo, jumla ya madarasa 85 yamekamilika, 30 yako katika hatua za mwisho na 9 yapo hatua za kati.

Alitaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa maabara 10 za sayansi katika Shule 5 za Sekondari ambao unatarajiwa kunufaisha jumla ya wanafunzi 450. Thamani ya miradi hiyo ni Shs. 590,585,220 ambapo maabara 8 zimekamilika na mbili ziko hatua za mwisho.

Miradi mingine iliyotekelezwa kupitia ufadhili kwa bajeti ya Serikali ni ujenzi wa nyumba 52 za walimu katika shule 13, Shule 7 zikiwa za Msingi na Shule 6 zikiwa za Sekondari.

Mradi huo, kwa mujibu wa Dkt. Kipesha, unatarajiwa kunufaisha jumla ya walimu 52 pamoja na familia zao, ambapo miradi hiyo yote kwa pamoja ina thamani ya Shs. 2,723,148,060 na kwamba nyumba zote zipo katika hatua za mwisho kukamilika.

“Mradi mwingine ni ujenzi wa matundu 888 ya vyoo katika Shule 37 zikiwemo Shule 29 za Msingi na Shule 8 za Sekondari. Mradi huu unatarajiwa kunufaisha jumla ya wanafunzi 21,312. Thamani ya miradi hii ni Shs. 2,065,357,904,” alifafanua Masuzi Nyirenda, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti wa Rasilimali na Miradi wa TEA.

Akaongeza kwamba, jumla ya matundu 120 yamekamilika, 600 yapo katika hatua za kukamilishwa na 168 yapo hatua ya kati.

Aidha, TE imefadhili ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule 8, ambapo saba ni za Msingi na moja ya Sekondari.

Miundombinu hiyo inahusisha madarasa 10, matundu ya vyoo 50, na mabweni 3, mradi unaotarajiwa kunufaisha jumla ya wanafunzi 2,010wenye mahitaji maalum.

Thamani ya miradi hiyo ni Shs. 609,334,224 ambapo miradi katika shule 4 imekamilika, shule 2 ziko katika hatua ya kukamilisha na shule 2 ziko katika hatua ya kati.

Pia kuna mradi wa ujenzi wa mabweni ya wasichana katika Shule 12 za Sekondari ambao unatarajiwa kunufaisha jumla ya wanafunzi wa kike 1,440 na wa kiume 120.

Gharama ya miradi hiyo ni Shs. 1,572,277,652 na mabweni 6 yamekamilika, matano yapo katika hatua za ukamilishaji (finishing stage) na moja katika hatua za awali.

Mradi mwingine ni wa ujenzi wa majengo 7 ya ofisi za walimu (majengo ya utawala) katika Shule 7 za Sekondari unaotarajiwa kunufaisha walimu 420 ambao unagharimu Shs. 754,085,080.

Kati ya hiyo, miradi miwili imekamilika, miwili iko hatua za ukamilishaji na mitatu hatua za kati.

Mamlaka hiyo pia imefadhili miradi kwa upande wa Zanzibar ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu pamoja na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika Taasisi mbili za Elimu ya Juu ambazo ni Chuo cha Sayansi na Teknolojia Karume (Karume Institute of Science and Technology-KIST) na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Kampasi ya Benjamin Mkapa-Pemba (State University of Zanzibar-SUZA, Benjamin Mkapa Pemba Campus).

Kulingana na Nyirenda, mradi huo unatarajiwa kunufaisha wanafunzi pamoja na watumishi (wahadhiri na wafanyakazi wasio wahadhiri) takriban 700 ambapo kwa pamoja miradi hiyo inagharimu Shs. 500,000,000.

“Mradi katika Chuo cha SUZA umekamilika, wakati Mradi wa KIST upo hatua za ukamilishaji,” alisema Nyirenda.

TEA pia imefadhili miradi kadhaa inayotekelezwa kwa pamoja na Wadau wa Elimu, ukiwemo ufadhili wa vijana 55 kusomea mafunzo ya Utalii na Ukarimu katika Chuo cha Hoteli na Utalii VETA (VHTTI) Arusha kwa gharama ya Shs. 55,980,000, kwa kushirikiana na Kampuni ya Asilia Giving.

Nyirenda anasema, mradi huo ni endelevu kwa kuwa wanafunzi wanasoma kozi ndefu.

Pia kuna ujenzi wa nyumba sita za walimu zenye thamani ya Shs. 150,000,000 katika shule ya Msingi Msinune, iliyopo Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani ambao ni wa ushirikiano kati ya TEA na Flaviana Matata Foundation ambapo nyumba 4 za walimu zimekamilika, na nyumba 2 zinatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka 2023/2024.

Kupitia Ufadhili wa TANAPA (kupita Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi), miradi kadhaa imetekelezwa ikiwemo ujenzi wa bweni la wavulana lenye kuchukua wanafunzi 120 kwa thamani ya Shs. 143,211,317 katika Shule ya Sekondari Kigonigoni, Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ambao tayari umekamilika.

Pia kuna ujenzi wa bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 kwa thamani ya Shs. 145,023,100 katika Shule ya Sekondari Kalemawe ya Halmashauri ya Wilaya ya Same ambao pia umekamilika.

Mradi mwingine ni ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu 12 ya vyoo katika Shule Shikizi ya Msingi Mgigiri iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, kwa thamani ya Shs. 77,157,931 ambapo madarasa na vyoo vimekamilika na madawati yapo hatua za ukamilishaji.

Mwaka 2023

Katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Mamlaka ya Elimu Tanzania imepanga kufadhili jumla ya miradi 82 ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule za Msingi na Sekondari kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Nyirenda, miradi hiyo itakapokamilika itanufaisha wanafunzi 39,484 na walimu 169 katika shule za msingi na sekondari.  

Aliitaja miradi itakayofadhiliwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa 82, matundu ya vyoo 336, mabweni 10, ujenzi wa maabara 18 za masomo ya sayansi na nyumba za walimu 32, miradi ambayo kwa sasa ipo katika hatua za awali za utekelezaji (Msingi na kujenga ukuta).

Mradi mwingine ni uboreshaji wa miundombinu na kuwezesha ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika taasisi moja ya elimu ya juu Tanzania Visiwani ambao umeanza rasmi mwezi Oktoba 2023 na unatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2024.

Miradi inayofadhiliwa na SDF

Dkt. Kipesha anasema, TEA pia imetekeleza miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (Skills Development Fund – SDF) ambapo kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2018/2019 hadi 2022/2023.

Anasema, jumla ya ruzuku ya kiasi cha Shs. 20,196,236,099.20 zimetumika kufadhili mafunzo kwa wanufaika 49,060 [Wanawake 22,410 (46%) na Wanaume 26,650 (54%)] ambao wamepatiwa mafunzo ya ujuzi katika sekta ya Kilimo na Kilimo Uchumi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Utalii na Huduma za Ukarimu, Nishati, Ujenzi na Uchukuzi.

“Kati ya vijana walionufaika, 464 walitoka kundi la wenye ulemavu, 2,928 walitoka kundi la vijana kutoka kaya masikini na wanaoishi katika mazingira magumu kwa upande wa Tanzania Bara na 600 walitoka kundi la vijana kutoka kaya masikini na wanaoishi katika mazingira magumu kwa upande wa Tanzania Zanzibar,” anasema Dkt. Kipesha.

Anasema, matokeo ya ufuatiliaji yamebainisha kuwa mafunzo yamewasaidia vijana kupata fursa za ajira, ambapo asilimia 80 ya wanufaika waliopata mafunzo wameweza kujiajiri au kuajiriwa.

Maeneo ya Kipaumbele katika ufadhili

Dkt. Kipesha anasema, maeneo ya kipaumbele katika ufadhili ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ikiwemo mabweni, nyumba za walimu, mabwalo na majiko, kumbi za mihadhara, madarasa, matundu ya vyoo, maktaba, maabara za sayansi na ofisi.

Lakini pia vifaa vya kufundishia na kujifunza ikiwemo vitabu, vifaa vya maabara, mashine na mitambo mbalimbali, vitabu vya kiada na zana nyingine za kufundishia.

Eneo jingine ni upatikanaji wa vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano – Tehama pamoja na kufunga mitandao, vifaa saidizi na vile vya kufundishia na kujifunzia wanafunzi wenye mahitaji maalum (wenye ulemavu), Programu maalum kuwezesha wanafunzi wa kike kujiunga na michepuo ya sayansi katika ngazi ya Vyuo Vikuu na Vyuo vya Ufundi, na mikopo kwa ajili ya ujenzi, upanuzi na ukarabati wa majengo kwa shule binafsi na vyuo vya elimu ya juu.

Mpango Mkakati

Dkt. Kipesha anasema, Tanzania imejipanga kutoa elimu bora na jumuishi inayozingatia Falsafa ya Elimu ya Kujitegemea iliyoasisiwa mwaka 1967 na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kupitia Sera ya Elimu iliyoboreshwa inayojumuisha Mtaala mpya.

Akasema, katika utekelezaji wa Mtaala mpya wa Elimu, TEA imejipanga kuhakikisha inaunga mkono utekelezaji huo kwa kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na upatikanaji wa vifaa ili kuongeza upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa nchini.

Safari ndefu

TEA ilianzishwa kwa Sheria ya Mfuko wa Elimu Na. 8 ya mwaka 2001 ikiwa na jukumu la kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa, Sheria ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2013.

Madhumuni ya Mfuko wa Elimu ni kuongeza nguvu za Serikali katika kugharimia miradi ya elimu ili kuinua ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa, katika ngazi zote za Elimu kwa Tanzania Bara na Elimu ya Juu kwa Tanzania Zanzibar.

Inaelezwa kwamba, kuanzia Oktoba 2017, Mamlaka pia ilipewa jukumu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia la kusimamia na kuratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (Skills Development Fund – SDF).

Mfuko huo ni sehemu ya Programu ya Kuendeleza Elimu ya Ujuzi na Mafunzo ya Stadi za Kazi zenye kuleta tija katika ajira (Education and Skills for Productive Jobs – ESPJ) na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza na Kuendeleza Ujuzi (National Skills Development Strategy – NSDS).

Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TEA kwa wahariri inasema, Mfuko wa SDF ulikuwa unatoa ufadhili wa mafunzo ya kuendeleza ujuzi katika sekta sita za kipaumbele zinazoratibiwa na Programu ya ESPJ, ambazo ni Kilimo na Kilimo Uchumi, Utalii na huduma za ukarimu, Uchukuzi, Ujenzi, Tehama na Nishati.

“Ufadhili na utekelezaji wa miradi ya Kuendeleza Ujuzi awamu ya kwanza ya ESPJ ulikuwa wa miaka mitano, kuanzia mwaka 2018/2019 ambao ulikamilika Juni 2023,” anasema Dkt. Kipesha.

TEA inalenga kuwa Mfuko wa Elimu bora wenye hadhi ya kimataifa unaotatua changamoto za elimu nchini, kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya mapato katika kuchangia maendeleo endelevu nchini.

Aidha, dhamira yake kubwa ni kutafuta rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya Mfuko wa Elimu na kuzigawa rasilimali hizo kwa ufanisi katika kufadhili miradi ya elimu ili kuboresha upatikanaji wa elimu bora na ujuzi kwa usawa, huku ikizingatia maadili ya kutekeleza majukumu yake kwa uwazi, uadilifu, uaminifu, weledi na kutoa huduma bora kwa wakati kwa wadau wote wa Mfuko wa Elimu kulingana na malengo ya Mamlaka.

TE ina majukumu makuu sita ambayo ni:

Kufadhili miradi ya elimu katika ngazi zote ili kuinua kiwango cha ubora wa elimu na kuongeza upatikanaji wake kwa usawa kulingana na mipango na sera za kitaifa kwa lengo la kukidhi mahitaji ya kijamii na kiuchumi;

Kuishauri serikali juu ya vyanzo vingine vya uhakika vya mapato kwa ajili ya Mfuko wa Elimu na kutafuta rasilimali kwa ajili ya Mfuko wa Elimu, ikiwa ni rasilimali fedha na/au vifaa kutoka katika vyanzo mbalimbali;

Kutayarisha na kutathmini mara kwa mara vigezo na taratibu za kutenga na kutoa fedha za Mfuko wa Elimu kwa ngazi zote za elimu nchini;

Kufuatilia na kuhakiki matumizi ya fedha za Mfuko zilizotolewa katika miradi ya elimu;

Kupokea zawadi, michango, hiba na rasilimali mbalimbali kwa ajili ya Mfuko wa Elimu; na

Kujenga ushirikiano na Taasisi za ndani na nje ya nchi kwa lengo la kushirikiana katika kuboresha elimu.

Vyanzo vya Mapato

Kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Elimu Na.8 ya Mwaka 2001, Sura ya 412 pamoja na marekebisho yake ya Mwaka 2013, vyanzo vya mapato vya TEA ni pamoja na: tengeo la kibajeti kwa ajili ya uendeshaji na Miradi ya Maendeleo; Tozo ya asilimia 2.5 ya ushuru wa forodha wa huduma za mawasiliano ya kielektroniki; na Kiwango kisichopungua asilimia 2 ya Bajeti ya Serikali ukitoa deni la Taifa.

Vynzo vingine ni Tengeo la Kodi ya Maendeleo ya Ujuzi (SDL) kwa mujibu wa sheria inayoanzisha Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi; na Vyanzo vingine ikiwemo, michango ya hiari kutoka kwa wadau mbalimbali, wafadhili wa miradi wa ndani na nje ya nchi, uwekezaji na mikopo yenye riba nafuu kwa taasisi za elimu.

Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2019/2020 hdi 2023/2024, Mamlaka hiyo imeendelea na utekelezaji wa makubaliano ya ufadhili wa wadau mbalimbali na kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia maendeleo ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu, ambapo kwa kipindi hicho jumla ya michango na ufadhili wa Shs. 1,444,284,034 ulipatikana.

Hiyo ni pamoja na michango ya fedha kutoka kwa wadau mbalimbali kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Taasisi ya Asilia Giving inayojihusisha na utalii jijini Arusha pamoja na Taasisi ya Flaviana Matata.

Pia mamlaka hiyo katika kipindi hicho ilipokea michango ya vifaa kutoka Yalin Global Company, Taasisi ya SAMAKIBA (Mbwana Samatta na Ali Kiba), Shirika lisilo la Kiserikali la Camara Education Tanzania,         Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania, Kampuni ya Baobab Shalom Limited, Darsh Industries Limited, Nissan Tanzania, Sayari Safi pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Licha ya kuwepo kwa changamoto, hasa za rasilimali fedha, lakini Mamlaka hii imeonyesha mafanikio makubwa ambayo kwa mazingira ya sasa na jitihada za Rais Samia, ni wazi kwamba miundombinu na mazingira ya kujifunzia na kufundishia yatakuwa bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *