TCB kuendelea kukuza sekta ya filamu, sanaa nchini

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imeshiriki katika kikao kazi cha uzinduzi wa Tamasha la Kimataifa la Maendeleo ya Filamu na Sanaa Tanzania linalotarajiwa kufanyika mwezi wa Desemba mwaka huu.

Tamasha hilo limeratibiwa na taasisi ya FAGDI (Foundation Ambassadors Gender Development Initiatives) ikishirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania. 

Tamasha hilo linawakutanisha wadau wa filamu na sanaa na wadau kutoka sekta mtambuka katika jukwaa moja kujadili mustakabali wa maendeleo ya sekta hiyo kitaifa na kimataifa.

Meneja Mkuu Kitengo cha Masoko wa benki hiyo, Janeth Zoya,  akizungumza mwishoni mwa wiki, kuhusu tamasha hilo alisema kutokana na changamoto nyingi zinazoikabili tasnia, litakuwa sehemu sahihi ya kuziwasilisha kupata ufumbuzi wake na kupanga mipango endelevu. 

“Benki ya TCB tunatambua nguvu iliyo nayo sanaa katika kuleta mabadiliko ndani ya jamii. Sanaa ni zaidi ya burudani ni chanzo cha kukuza uchumi, kuchochea umoja wa kitaifa na kutambulisha utamaduni wetu duniani. Tasnia ya filamu na sanaa ina uwezo mkubwa wa kutuvusha nje ya mipaka, kusimulia hadithi na urithi wetu, na kuonyesha ufahari wa tamaduni za Kitanzania duniani,” amesema. 

Zoya ameendelea kusisitiza umuhimu wa tamasha hilo akisema, “Tamasha hili litatoa fursa muhimu ya kuwakutanisha pamoja wadau mbalimbali kujadili mikakati itakayokuza uchumi na maendeleo ya sekta hii. Hivyo, ni vizuri kutumia fursa hii kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta, zikiwamo zile zinazohusiana na uwezeshwaji, uelimishaji na upatikanaji wa masoko. 

“Lakini la muhimu zaidi, tunapaswa kutambua fursa zilizopo mbele yetu – uwezekano wa kufanya ushirikiano kimataifa, matumizi ya majukwaa ya kidigitali ili kuifikia hadhara ya kimataifa na kutengeneza muundo endelevu utakaowezesha mafanikio ya muda mrefu.” 

Udhamini wa Benki ya TCB katika uzinduzi huo unaimarisha dhamira yake ya kusaidia miradi mbalimbali inayochangia maendeleo ya utamaduni na uchumi nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *