Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI maarufu ya Michezo ya Kubashiri ya betPawa, imetangaza udhamini wa shilingi 194,880,000 kwa Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL), inayoendelea sasa katika Mkoa wa Dodoma.
Kwa mujibu wa Ofisa Mkuu wa Biashara wa betPawa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Michezo, Ntoudi Mouyelo, wameamua kudhamini mpira wa kikapu nchini ili kusaidia kukuza mchezo huo.
Mouyelo ameeleza sh. milioni 130 zimetengwa kwa ajili ya “Locker Room Bonus” na sh. milioni 14 kwa zawadi za ushindi, na fedha zinazobaki zitasaidia usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF).
Amesema betPawa ilichagua kudhamini ligi hiyo na kusaidia TBF kutokana na utawala wake mzuri na uwazi.
“Kampuni yetu imejidhatiti katika kukuza mchezo pamoja na kusaidia jamii,” ameongeza Mouyelo.
Mouyelo pia ameanzisha “Locker Room Bonus” katika NBL, mfumo wa zawadi kwa wachezaji, ambapo wachezaji 12 na maofisa wanne wa timu inayoshinda wanapokea sh. 140,000 kila mmoja.
Bonasi hiyo italipwa moja kwa moja kwenye akaunti za simu za wachezaji mara baada ya ushindi na kabla ya wachezaji na wafanyakazi kuondoka uwanjani, hivyo jina “Locker Room Bonus.”
Mbali na Locker Room Bonuses, betPawa imejitolea shilingi milioni 14 kugawanywa kwa wachezaji bora na timu itakayoshinda mwishoni mwa msimu wa 2025.
“Tunalenga kuukuza mpira wa kikapu katika kanda hii, kama tulivyofanya Rwanda kupitia ushirikiano kama huu na FERWABA (Shirikisho la Mpira wa Kikapu Rwanda),” amesema Mouyelo.
Mouyelo ameongeza betPawa itasaidia mshindi wa NBL katika Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Afrika inayofuata.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa, na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Tamba Boniface, amesema msaada huo unaonesha imani ya betPawa kwa vipaji, uwezo na mustakabali wa mpira wa kikapu nchini Tanzania.
Mwinjuma amesema kudhamini ligi na kuanzisha mipango kama Locker Room Bonus kunachochea ndoto za wanamichezo chipukizi na kuendeleza utamaduni wa michezo unaokua nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Rais wa TBF, Michael Kadebe, ameishukuru betPawa kwa udhamini na kuahidi kutumia fedha hizo kama zilivyoelekezwa.