
Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
CHAMA cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) mwaka huu, kinaadhimisha miaka 35 ya mafanikio makubwa katika kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto wa kike nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA Tike Mwambipile, ametangaza mafanikio hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati akieleza kuhusu kongamano kubwa litakalofanyika Mei 22 na 23 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Dotto Biteko.
Amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 1989 na kusajiliwa rasmi mwaka 1990, TAWLA imekuwa kinara katika utoaji wa msaada wa kisheria, utetezi wa kisera, elimu kwa umma na tafiti zinazolenga kuimarisha usawa wa kijinsia.

Amesema katika kipindi hicho wamefanikiwa kufungua ofisi zake sita zilizopo Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza, Mbeya na Tanga, TAWLA imefanikiwa kuwafikia zaidi ya watu milioni 7 kwa huduma za kisheria.
“Pia imekuwa chachu ya mabadiliko katika sheria na sera mbalimbali, ikiwamo Sheria ya Mtoto ya 2009, Sheria ya Ardhi, na jitihada za kubadilisha Sheria ya Ndoa ya 1971 ili kuzuia ndoa za utotoni,” amesema Tike.
Katika juhudi zake, TAWLA imewezesha wanawake zaidi ya 400 kupata hati miliki ya kimila na kufanikisha upitishaji wa sheria ndogo zenye mlengo wa kijinsia katika vijiji 178.
Aidha, amesema zaidi ya wanawake 500 wamepatiwa mafunzo ya uongozi na kushiriki katika nafasi mbalimbali za maamuzi.Maadhimisho hayo pia yameambatana na uzinduzi wa ofisi mpya mkoani Dodoma na maandalizi ya kongamano hilo litawajumuisha wadau mbalimbali kujadili masuala muhimu ya haki za wanawake na watoto wa kike.
Ametaja mada hizo ni ndoa za utotoni, usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi na elimu kwa wasichana waliopata ujauzito.
“Katika kuelekea miaka ijayo, TAWLA imejipanga kupanua huduma vijijini, kutumia teknolojia kufikisha msaada wa kisheria na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali. Shirika linatoa wito kwa serikali, taasisi na jamii kushirikiana kuendeleza ajenda ya kitaifa ya haki na usawa,” amesema.