Tanzania yaunga mkono China ujenzi miundombinu wezeshi

Na Benny Mwaipaja, Beijing

TANZANIA imeunga mkono hatua ya China ya kusisitiza umuhimu wa kutumia njia mbadala ya kutoa mikopo na misaada kwa nchi zinazoendelea zikiwemo za Afrika kwa kuishirikisha sekta binafsi ili kuchochea kasi ya ujenzi wa miundombinu kupitia mpango wake wa Belt and Road Initiative (BRI).

Kauli hiyo imetolewa Jijini Beijing, nchini China na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maanry Mwamba, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Tatu la Kimataifa la Belt and Road Initiative, ulioyakutanisha mataifa kadhaa duniani, ukibeba kaulimbiu ya kuimarisha uchukuzi ili kukuza Biashara (Trade & Connectivity’)

Amesema kuwa utaratibu wa mikopo katika mazingira ya sasa ambapo mwenendo wa madeni ya Serikali kwa nchi nyingi za Afrika ni changamoto kubwa, utaratibu wa ubia kati ya sekta ya Umma na Sekta binafsi- PPP katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu wezeshi ya biashara, unafaa zaidi.

Ripoti ya Jukwaa la kiuchumi la Kimataifa- World Economic Forum- 2018 inaonesha kwamba zaidi ya asilimia 80% ya Biashara Duniani inafanyika kupitia Bahari, huku Tanzania ikitajwa na Benki ya Dunia kama moja ya lango la kimataifa ambapo takribani nchi 6 zinazoizunguka ambazo hazina bahari, zinategemea kufanya biashara na Dunia kupitia Tanzania.

Akizungumzia mipango ya Serikali katika kukuza agenda ya biashara na ujenzi wa miundombinu, Dkt. Mwamba alisema kuwa Tanzania inatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa, Viwanja vya ndege, Bandari, na miundombinu ya barabara ambayo imelenga kukuza biashara na uchumi wa nchi.

Alisema kuwa mpango wa Belt and Road Initiative ni muhimu kwa Tanzania ambapo kwa kutumia mikopo nafuu, misaada na utaratibu mwingine wa kutekeleza miradi kwa njia ya PPP (Altenative Financing), utaiwezesha nchi kunufaika kwa kujenga miundombinu hiyo kwa ajili ya ustawi wa Taifa na kutumia mapato yake ya ndani kuendeleza huduma nyingine za jamii.

Mpango wa Belt & Road Initiative uliasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jimping miaka kumi iliyopita kwa ajili ya kuziwezesha nchi kujenga miundombinu itakayochochea ukuaji wa biashara miongoni mwa mataifa ya dunia ambapo kiasi cha dola za Marekani trilioni 1 kitatumika kuwezesha mpango huo.

Malengo ya Mhe. Rais Xi Jimping ni kuutambulisha utamaduni wake na kuifanya ishike hatamu katika suala zima la biashara na uwekezaji kwa kuweka miradi mikubwa ya miundombinu katika nchi zinazohusika kwenye maeneo yaliyopitisha biashara hizo, ambayo inajumuisha ujenzi wa Bandari, Viwanja vya ndege, Vinu vya kufulia umeme na njia za kuusambazia, Reli, Mabwawa Makubwa ya kuhifadhia maji, Barabara, Kanda maalum za viwanda na biashara (Industrial parks).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *