Tanzania yakipigia chapuo Kiswahili kitumike mikutano ya Benki ya Dunia, IMF

Na Benny Mwaipaja, Marrakech

TANZANIA imeishauri Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kukifanya Kiswahili kuwa miongoni wa lugha za mawasiliano wakati wa mikutano yake kutokana na kukua kwa lugha hiyo, kutumika katika mikutano mingine mingi ya kikanda na kimataifa.

Ushauri huo umetolewa Mjini Marrakesh nchini Morocco na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum.

Dkt. Mkuya alitoa ushauri huo kwenye Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Fedha, Magavana wa Benki Kuu kutoka kundi la kwanza la nchi za Afrika ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia.

Katika mkutano huo, Dkt. Salum ndiye anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia na IMF, kwa niaba ya Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Alisema ni wakati muafaka wa kukijumuisha Kiswahili katika mijadala ya taasisi hizo kubwa za fedha duniani, wanachama wake wengi kutoka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wanazungumza lugha hiyo.

“Takribani watu milioni 200 wanazungumza Kiswahili duniani, tumewasilisha ombi hili ikiwa ni jitihada za Serikali kukibidhaisha Kiswahili kama ilivyo kwa lugha nyingine rasmi zinazotumika kwenye mikutano ya Benki ya Dunia na IMF,” alisema Dkt. Salum.

Agenda hiyo itajadiliwa wakati wa Mkutano wa 27 wa kundi la kwanza la nchi za Afrika ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia, wakati wa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na IMF, itakayofanyika Washington D.C, nchini Marekani, Aprili, 2024.

Katika mkutano wa 26 wa kundi la kwanza la nchi za Afrika, wajumbe waliiomba Benki ya Dunia kutoa fedha ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwezeha biashara ya hewa ukaa.

Pia kusaidia bajeti za nchi wanachama, kuongeza kiwango cha fedha za mikopo nafuu, misaada kwa nchi zinazoendelea ili kutekeleza miradi ya maendeleo.

Waliitaka benki hiyo kuzihudumia nchi wanachama wake kwa usawa wakati wa majanga ikiwemo matatizo ya mizozo ya kivita kama wanavyofanya kwenye nchi nyingine zenye matatizo kama hayo kwenye mabara mengine.

Hatua hiyo inakwamisha juhudi za nchi hizo kukabiliana na changamoto hizo na kujikwamua kiuchumi.

Mkutano huo umehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ambaye pia ni Gavana mbadala wa Tanzania katika Benki ya Dunia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Amina Khamisi Shaaban. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *