Na Sarah Moses, Dodoma.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa na Mwenyeki wa Kamati ya Kitaifa ya Mashindano ya Chan na Afcon 2027 amesema Tanzania imejipanga kulibakiza kombe la Chan 2025 kutokana na maandalizi yaliyowekwa na serikali kwa kushirikiana na shirikisho la mpira wa miguu nchini.
Hayo ameyasema leo Februari mosi ,2025 jijini hapa wakati akizungumza na Wabunge na wanamichezo katika bonanza la Azania Bunge Bonanza lililohusisha mashabiki wa Simba na Yanga.
“Maandalizi yetu siyo kushiriki tu katika mashindano hayo bali tumejiandaa na inawezekana pasiposhaka kulibakiza kombe hilo nyumbani, naomba Watanzania wafahamu hilo uwezo tunao kwasababu hata ligi yetu imeendelea kuwa bora Afrika,” amesema.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya michuano hiyo Majaliwa amesema maandalizi yanaenda vizuri hasa katika miundombinu ya michezo lakini wakaguzi wa viwanja walipofika nchini wameridhika na maandalizi hayo.
Katika hatua nyingine Majaliwa amewaasa wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kutokomeza magonjwa yasiyokuwa yakuambukiza.
Kwa upande wake Spika wa Bunge Dk.Tulia Ackson amesema wataendelea kuongeza ubunifu katika mabonanza yanayokusanyisha wabunge na wananchi ili kuvutia watu wengi zaidi kushiriki kwa manufaa yao.
“Ubunifu wa kufanya Yanga na Simba ni kwa mara ya kwanza tunafanya lengo ni kuendelea kuongeza ubunifu ili kuvutia wananchi wengii zaidi kushiri. Na bonanza la mwaka huu limekuwa na mwamko mkubwa kwasababu washiriki wengine wametoka majimboni kuja kushiriki,”amesema.
Kwa upande wake Ofisa Matekelezo Mwandamizi kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Ritha Nguruwe amesema mazoezi ni muhimu kwa watumishi ambao muda mwingi wanautumia wakiwa wamekaa kwani yanasaidia kuepusha na magonjwa yasiyo yakuambukiza.
“NSSF tumeshiriki katika bonanza la Azania Bunge Bonanza lengo ni kuendelea kuhamasisha watumishi kufanya mazoezi kwasababu ni muhimu kwa afya hasa kwetu sisi watumishi ambao muda mwingi kazi zetu tunazifanya tukiwa tumekaa,”amesema.
Mwisho.