Tanzania ya tatu mazingira bora ya uwekezaji Afrika

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, amesema kulingana na tafiti za kimataifa, Tanzania ni nchi ya tatu kwa ubora kuwa na mazingira mazuri ya Uwekezaji barani Afrika, ikitanguliwa na Nigeria, Afrika Kusini.

Prof. Mkumbo aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa Jukwaa la Biashara lililowakutanisha wawekezaji kutoka Tanzania na Ujerumani.

Alisema maboresho yaliyofanyika katika sheria, sera, kiutumishi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiyo msingi wa matokeo hayo kwa Tanzania.

Alieleza kuwa, maeneo aliyojadiliana na Ujerumani wanayoweza kuwekeza ni pamoja na nishati jadilifu, kuzalisha umeme wa maji, jua, upepo.

Pia uzalishaji wa madini ya kimkakati ya kutengeneza betri na kuunganisha magari ikiwemo Volkswagen.

“Tunataka Tanzania ichukue nafasi yake katika ukanda Afrika, kuwekeza viwanda vya kutengeneza magari,” alisema Prof. Mkumbo.

Aliongeza kuwa, ujumbe huo umetoa pongezi zao kwa Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji pia wameiomba Serikali iendelea kuboresha masuala ya nishati na bandari.

Kongamano hilo limejumuisha viongozi wa Serikali na wawekezaji wa kutoka Ujerumani na Tanzania.

Ujerumani ni miongoni mwa nchi kumi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini.

Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), hadi kufikia Agosti, 2023, Ujerumani imewekeza katika miradi 178 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 408.11 na kutoa fursa za ajira 16,121.

Ilibainishwa kuwa, kampuni za Ujerumani zimewekeza katika sekta kadhaa za uchumi wa Tanzania kama kilimo, ujenzi, taasisi za kifedha, uzalishaji, uchimbaji madini, huduma za usafirishaji, nishati, mawasiliano, utalii na maliasili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *