Na Bwanku Bwanku.
Kila ikifika Mei 03, 2023 ni Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambapo Tanzania iliungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku hii.
Kitaifa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani mwaka huu yalifanyikia Zanzibar kwenye Ukumbi wa Golden Tulip Mkoa wa Mjini Magharibi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi alikuwa mgeni rasmi.
Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu inayosema ‘Kuunda Mustakabali wa Haki – Uhuru wa Kujieleza kama kichocheo cha Haki nyingine za Binadamu’.
Dkt. Mwinyi kwenye hotuba yake amesema Tanzania sasa inashuhudia usajili mkubwa wa vyombo vya habari kuliko kipindi chochote kile katika historia na kusema kwamba Serikali inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kutoa elimu, amani, mshikamamo na kuweka taswira nzuri ya Taifa Nje huku ikifichua vitendo viovu pia.
Kifupi ni hivi, Sekta ya Habari ni moja ya Sekta muhimu sana kwenye Maendeleo na Uchumi wa Taifa lolote lile Duniani. Kwa lugha isiyo rasmi, Sekta ya Habari inachukuliwa kama Mhimili wa 4 wa Taifa usio rasmi na usioonekana ambao umekuwa daraja kubwa sana kati ya Wananchi na Serikali kupitia kusukuma ajenda za Maendeleo, Kijamii, Uchumi, utamaduni na kadhalika wa kadhalika.
Katika kipindi hiki cha ukuaji mkubwa wa Sekta hii ya Habari Duniani uliochangiwa kwa kiwango kikubwa na Mapinduzi makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Utandawazi, leo changamoto mbalimbali za Kiuchumi, ubadhirifu, ufisadi, changamoto za kijamii, miundombinu, kijinsia, unyanyasaji na zingine zimekuwa zikipaziwa sauti na kupatiwa ufumbuzi haraka na Wananchi kupata huduma vyema kupitia ushawishi ulionao Sekta ya Habari kufikisha ujumbe kwa Mamlaka za Serikali na zingine.
Tumeshuhudia mara nyingi jambo baya au lisilo na taswira njema kwenye Jamii na linaloumiza Wananchi likiibuliwa kwenye mitandao ya Kijamii na kwenye Vyombo vya Habari na papo hapo mara moja Serikali ikichukua hatua ya kutatua na kuchukua maamuzi. Hii pekee ukiachana na mengine mengi yanayofanywa na Sekta hii ya Habari inaonyesha umuhimu mkubwa wa Sekta hii.
Kwa kutambua unyeti na umuhimu wa Sekta hii ya Habari kwenye Maendeleo na ukuaji wa Uchumi wa Taifa lolote likwemo Tanzania, Serikali ya Tanzania imeendelea kuipa Sekta hii inayotajwa kuwa Mhimili wa 4 wa Nchi usio rasmi umuhimu mkubwa sana kwa kuzidi kuimarisha mifumo yake ya utendaji kazi, kuvihakikishia Uhuru wake wakati wa kutekeleza majukumu yake, kuangalia sheria zinazoonekana au kulalamikiwa kubana Uhuru wake, kupunguza tozo kwenye maeneo mbalimbali pamoja na kuangalia maeneo mengine mengi ya msingi ili kuiboresha Sekta hii, Mhimili usio rasmi wa 4 ndani ya Taifa.
Hii yote ni katika kuhakikisha Sekta hii inachangia Maendeleo ya Taifa, inaibua fursa mbalimbali zilizopo kwenye Jamii na kuzitangaza kwa Wananchi, kuibua maovu ndani ya Jamii, kero, changamoto, kuzalisha ajira kwa Watanzania wanaofanya kazi kwenye Sekta hii na mengine mengi.
Licha ya changamoto za hapa na pale lakini haiondoi ukweli kwamba Tanzania ni moja ya Mataifa machache Afrika na pengine Duniani yenye Uhuru mkubwa sana wa Vyombo vya Habari. Hili unaweza kulipima hata kwa kipimo kidogo cha kuangalia hali ya Uhuru vya Vyombo vya Habari kwa kuangalia hata idadi ya Vyombo vya Habari hapa nchini.
Kwa Takwimu za Idara ya Habari Maelezo inayolea na kusimamia Sekta hii, Tanzania mpaka sasa ina Jumla ya Magazeti na Majarida 257, Vituo vya Redio 200, Televisheni 46, Redio za mtandao 24, Televisheni za Mtandao (Online TV) 474, Blogs 63, Website 123 na Majukwaa ya mijadala ya mitandaoni 2. Hili linawezekana pekee kwenye Taifa lenye Uhuru mkubwa wa Vyombo vya Habari na kamwe haliwezi kutokea kwenye Taifa linalominya Uhuru wa Vyombo vya Habari ama kwenye Taifa linaloendeshwa Kidikteta.
Hii pekee inakuonyesha namna Taifa linavyoipa Uhuru mkubwa Sekta hii na ndiyo maana kumekuwa na ongezeko kubwa la Vyombo vya Habari kila kukicha kutoka viwili tu vya Uhuru na Daily News wakati tunapata Uhuru Mwaka 1961 mpaka idadi hii kubwa tuliyonayo sasa na hii ni kwasababu tu ya ukweli kwamba hayupo anayeweza kukubali kuanzisha chombo cha Habari kama hakuna Uhuru na kuna mizengwe ya uendeshaji wake kutoka kwa Serikali, hivyo uwingi wake huu mkubwa unadhirisha Uhuru mkubwa na uimara wa Sekta hii nchini.
Hapa tunapozungumza, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari chini ya Waziri wake Mhe. Nape Nnauye imeshachukua hatua mbalimbali za kuangalia maeneo mbalimbali yanayokwamisha Uhuru wa Habari ikiwemo sheria, taratibu, ada za leseni ya Vyombo vya Habari, masuala ya uendeshaji wake.
Tayari Sheria mbalimbali zinazolalamikiwa na Wadau mbalimbali kuvibana Vyombo vya Habari kufanya shughuli zake kwa weledi zimeanza kumulikwa na kuanza utaratibu wa kuziboresha ama kuzibadiri ikiwemo kuiangalia hii Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari (The Media Services Act) ya Mwaka 2016 inayolalamikiwa na tayari Serikali imeshaanza kukutana na Wadau wa Sekta hii kuangalia namna ya kuiboresha na kuifanyia marekebisho na hivi karibuni Muswada wa Sheria ya Habari utapelekwa Bungeni kujadiliwa na kuboreshewa.
Pia, Serikali imechukua uamuzi wa kupunguza ada ya kuanzisha Televisheni za mtandao (Online TV) kutoka zaidi ya Laki 5 ya zamani mpaka chini ya Laki mbili kuelekea elfu 50 ili tu kutengeneza mazingira ya Vyombo vingi zaidi kuanzishwa ili kupeleka taarifa kwa Wananchi na zaidi kutengeneza ajira kwa kundi kubwa la Vijana wanaokimbilia kila kukicha Sekta hii na waliojiajiri kwenye Sekta hii inayokua kwa kasi kubwa sana Duniani.
Kwahiyo, wakati huu tukiwa kwenye Wiki ya kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye eneo hili, tukishuhudia idadi kubwa sana ya Vyombo vya Habari pengine kuliko Taifa lolote jirani na sasa Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Rais Samia ikiweka mkazo mkubwa sana kwenye kumulika changamoto mbalimbali nilizozitaja.