Na Mwandishi Wetu
ZAIDI ya wafanyabiashara 3,000 kutoka Tanzania na wengine zaidi ya 3,000 kutoka Uingereza, wamejisajili kwenye Tanzania Link Portal ambayo ni jukwaa la kidijitali linalolenga kuimarisha fursa za kiuchumi kati ya Tanzania na Uingereza kupitia ushirikiano wa biashara, uwekezaji, elimu, utalii na ajira.
Tanzania Link ni ubunifu wa Watanzania watatu wanaoishi Uingereza, Goodluck Mboya, Joseph Ndilla na Bi Shivani Patel, walioanzisha jukwaa hilo kwa lengo la kusaidia kufungua milango ya ushirikiano kwa Watanzania walioko nyumbani na wale waishio diaspora pamoja na washirika wao kutoka Uingereza.
Tovuti yao ilizinduliwa rasmi Aprili, mwaka huu na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika hafla maalum jijini London, Uingereza.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mbelwa Kairuki, Mama Mariam Mwinyi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Cosato Chumi, Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Mizengo Pinda pamoja na wanadiaspora na wadau wa maendeleo kutoka sekta mbalimbali.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Biashara wa Tanzania Link, Joseph Ndilla, amesema jukwaa hilo limepokelewa kwa muitikio mkubwa na tayari baadhi ya wafanyabiashara kutoka Tanzania na Uingereza wameanza mazungumzo ya ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji.
“Kupitia Tanzania Link, tunawawezesha wafanyabiashara kupata taarifa na kushiriki katika fursa za uwekezaji wa moja kwa moja, ubia wa kibiashara, masoko ya kimataifa na hata nafasi za ajira katika sekta mbalimbali. Pia tunasaidia Watanzania kupata taarifa sahihi kuhusu udhamini wa masomo (scholarships) na programu za ubadilishanaji wa kitaaluma na kielimu,” amesema Ndilla.
Aidha, amesema Tanzania Link inatoa mwongozo na msaada wa kisheria kwa wafanyabiashara wapya, wajasiriamali na wawekezaji wanaotaka kufanya kazi kati ya Tanzania na Uingereza, huku jukwaa hilo likitoa taarifa za utalii wa Tanzania Bara na Zanzibar kwa wageni kutoka Uingereza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi, Goodluck Mboya, ameeleza Tanzania Link siyo tu jukwaa la kidijitali bali ni daraja la kimkakati linalounganisha watu, fikra na mitaji.
“Tanzania Link ni jukwaa la kizalendo lenye mtazamo wa kimataifa. Ni ishara ya mshikamano wa Watanzania duniani kote katika kujenga uchumi jumuishi. Tunachangia kwa vitendo utekelezaji wa diplomasia ya kiuchumi inayoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Mboya.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania Uingereza, Mbelwa Kairuki, amesema Tanzania Link ni jukwaa linaloendana na malengo ya kisera ya serikali ya kukuza diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kimataifa.
“Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza unalipokea kwa mikono miwili na utaendelea kushirikiana kwa karibu na waanzilishi wake ili kuhakikisha mafanikio ya jukwaa hili kwa manufaa ya Watanzania na washirika wao wa maendeleo,” amesema Balozi Kairuki.