
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema, Tanzania itakua kwenye ramani ya dunia kama moja kati ya wachangiaji 10 wakubwa zaidi wa malighafi ya madini ya Urani kwenye nishati safi.
Hayo yamebainishwa jana na Rais Samia wakati akizungumza na wananchi baada ya kuzindua kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji wa madini ya Urani kilichopo Namtumbo mkoani Ruvuma.
Amesema kutekelezwa kwa mradi huo wa majaribio, ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Taifa ya kuifanya Tanzania kuwa Taifa lenye viwanda na kufikia matarajio ya uchumi wa kati ngazi ya juu unaojitegemea.
Amesema historia imeandikwa kutokana na kuzinduliwa kwa mradi huo ikiwa ni siku ya ushindi wa juhudi za siku nyingi kutafuta njia sahihi salam na zenye manufaa za taifa katika kutumia rasilimali zilizopo hasa madini hayo.
Amesema madini ya Urani ni kati ya madini ya kimkakati duniani yanayotumika katika kuzalisha nishati ya nyuklia, tiba za saratani na tafiti za kisayansi za hali ya juu.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ndani ya bara la Afrika zilizobarikiwa kuwa na akiba ya madini ya Urani na taarifa za kitaalamu zinaonesha kuwa maeneo ya Mkuyu ambapo hapa Namtumbo ni sehemu yake yenye uwezo wa kuzalisha tani 300,000 kwa mwaka,” amesema.
Amesema hiyo ni hazina kubwa yenye thamani kiuchumi, kisayansi na kimkakati ambapo kupitia mradi huo, Tanzania inajiweka katika nafasi ya kuwa kitovu cha utafiti na uchakataji wa Urani kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
Amefafanua kuwa inasemekana ndani ya Bara la Afrika unashikiliwa takribani asilimia 20 ya hifadhi ya Urani Duniani ambapo inachakatwa kwa asilimia ndogo.
Ameongeza kuwa kuzinduliwa kwa mradi huo kunaifanya Tanzania kuchangia katika uchakataji na uongezaji thamani wa rasilimali zake ndani ya nchi na Bara la Afrika.
Rais Samia amesema kiwanda hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya nchi ya kuhakikisha madini hayo yanatumika kwa manufaa ya watanzania wote kwa kuzingatia usalama wa kiafya, kimazingira na kufuata viwango vya kimataifa.
Anaongeza kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ni mchango mkubwa katika juhudi za serikali za kuhakikisha madini yanatoa mchango mkubwa wa kuzalisha ajira.
Anasema tathmini iliyofanywa inaonesha mradi huo utazalisha kwa zaidi ya miaka 20 ambapo katika kipindi hicho Tanzania itanufaika na uwekezaji wa fedha za kigeni dola za Marekani bilioni 1.2, ajira hadi 4000 katika kipindi cha ujenzi wa miundombinu, ajira 750 za kudumu na zingine 4,500 kutokana na shughuli nyingine katika eneo hilo.
“Serikali inakadiriwa kupata mapato ya mradi Dola za Marekani milioni 373, kodi ya miti dola milioni 26, kodi ya zuio dola milioni 15.7, tozo ya leseni, dola milioni 20.8, kodi ya makampuni dola bilioni 1.01 na gawio la serikali asilimia 20 sawa na dola milioni 40 kwa mwaka,”amesema.
Rais Samia ametoa rai kwa kampuni ya uchimbaji kuzingatia ushirikishwaji wa Watanzania na wajibu wa kampuni kwa jamii kama ilivyoainishwa kwenye sheria ya madini.
“Kipaumbele cha ajira kiwe kwa watanzania na hususan wananchi waliopo katika vijiji na maeneo yaliyo karibu na mradi kwa ajira zisizo hitaji ujuzi mkuba,”amesema Rais Samia.
Ametoa wito kwa Wizara ya Madini kupitia taasisi zote zinazosimamia na kuhusika na mradi huo kuhakikisha mradi unakua shirikishi, endelevu na kutoa manufaa makubwa kwa watanzania.
Amewataka wananchi wa Namtumbo kuupokea mradi huo kwa mikono miwili ambao utasaidia kukuza uchumi wa Mkoa, kukuza huduma za kijamii ikiwemo maji, barabara, maji, shule vitaboreshwa kwa kuzingatia shughuli za kiuchumi.
Amesema mradi huo utavutia wawekezaji na kuongeza thamani ya madini ya urani katika mnyororo wa uchumi wa Wilaya hiyo.
Amewataka wenye madai kuhusu mradi huo, kuyapeleka serikalini na si kwenye mradi ili hatua zichukuliwe.
Amesema tathmini ya kimkakati za maizngira imekamilika na kuruhusu mradi huo kuendelea ambapo alisisitiza kampuni ya Mantra kuzingatia masharti yote yaliyotolewa kupitia tathimini hiyo na serikali kuendelea kusimamia uendelezaji wa mradi huo kwa mujibu wa masharti hayo.
Amesema kutokanana na Tanzania kuchimba madini hayo kwa mara ya kwanza, ni lazima taasisi zinazohusu mazingira zijipange ipasavyo.
Ametoa wito Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, Tume ya nguvu za Atomic Tanzania kulisimamia ipasavyo ili kulinda mazingira na Watanzania.
Rais Samia amesema mahitaji ya matumizi ya madini ya Urani yameongezeka hasa kuzalisha umeme wa nguvu ya nyuklia.
Amesema katika kipindi cha miaka 25 ijayo ni muhimu kuangalia fursa za kuzalisha umeme kutokana na vyanzo vingine ikiwemo madini ya Urani lengo likiwa kuwa na vyanzo mesto vya madini ya Urani ili kujihakikishia usalama wa nishati.
Amesema sekta ya madini imepanda na kuongeza mchango katika pato la taifa ambapo mwaka 2021 sekta hiyo katika pato la taifa imekua kutoka wastani wa asilimia 7.3 hadi kufikia wastani wa asilimia 10.1 mwaka 2024.
Rais Samia ameongeza kuwa, ukuaji wa sekta ya madini umepandisha ukuaji wa mapato ya serikali yanayotokana na shughuli za uchimbaji madini.
Ametoa wito kwa Wizara ya Madini kuwa makini kuhakikisha wanasimamia na kuchochea ukuaji wa sekta hiyo kwa manufaa ya watazania na taifa kwa ujumla.
“Hatuna budi kuzitumia fursa zitokanazo na mradi kama huu tuliouzindua leo, katika mradi huu licha ya ajira za ndani kutakua na mahitaji kadhaa ya uendeshaji wa mgodi lakini pia kiwanda,”anasema.
Amefafanua kuwa pia kutakua na mahitaji binafsi kwa watu watakaokua na shughuli mbalimbali katika eneo hilo la mradi.
Amewataka wananchi kuchangamkia fursa hizo kujenga uchumi wao
Amesema serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji katika kufanikisha ukamilishaji wa mradi huo.



