Tanzania, India kukuza uhusiano wa kimkakati

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akiagana na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, mara baada ya mapokezi katika Ikulu ya India Oktoba 9, 2023

Na Mwandishi Wetu,

India

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na India zimekubaliana kukuza uhusiano wao wa kihistoria baina ya mataifa hayo mawili kwa kiwango cha Ushirika wa Kimkakati.

Rais alisema ziara yake ya kiserikali inasisitiza dhamira ya serikali yake ya kuimarisha na kudumisha urafiki na ushirikiano baina ya Tanzania na India, ambao umekuwepo kwa miongo kadhaa.

Rais Samia aliyasema hayo jana Jumatatu, Oktoba 9, 2023 wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika ziara yake ya kitaifa ya siku tatu nchini India.

Alisema miongoni mwa masuala ambayo viongozi hao wameyawekea msisitizo katika ushirikiano ni ulinzi, nishati, kujenga uwezo, usalama wa majini, biashara na uwekezaji.

Rais Samia alisema mazungumzo ‘ya wazi na ya kirafiki’ na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, yalisisitiza shauku ya pande zote mbili na kujitolea kuimarisha na kuongeza uhusiano wa nchi hizo mbili kwa viwango vya juu zaidi.

“Tumekubali kufungua njia mpya za ushirikiano na kuongeza ushirikiano wetu kwa mfumo wa Ushirikiano wa Kimkakati,” Rais Samia alisema katika mkutano na waandishi wa habari na Modi katika mji mkuu wa India, New Delhi, baada ya mazungumzo ya pande mbili.

Akielezea India ‘kama mwanafamilia mkubwa’ Rais Samia alibainisha kwa kuridhika kwamba kiasi cha biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili kilikuwa katika hali ya juu.

“Hadi kufika mwaka 2022, kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili ulifikia dola za Kimarekani bilioni 3.1 hivyo kuifanya India kuwa mshirika wa tatu kwa ukubwa katika biashara na mwekezaji wa tano kwa ukubwa nchini Tanzania,” alisema.

Mkuu huyo wa Nchi alisema Tanzania na India pia zinashirikiana katika maeneo mengine kadhaa, akitolea mfano maji safi na salama, ulinzi na usalama.

Rais Samia alimpongeza Modi kwa kuandaa Mkutano wa G20 mjini New Delhi mwezi uliopita ambapo Waziri Mkuu wa India alifanikiwa kutetea Afrika kuwa mwanachama kamili wa G20, mapendekezo ya msamaha wa madeni kwa mataifa yaliyo hatarini, mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, taasisi za fedha za kimataifa na Shirika la Biashara Duniani (WTO).

Rais Samia alishukuru uamuzi wa India kufungua kampasi ya kwanza ya Taasisi ya Teknolojia ya India (IIT) nje ya India, chuo chenye hadhi ya juu katika masuala ya teknolojia, visiwani Zanzibar kitakachowanufaisha wanafunzi mbalimbali si tu wa Tanzania ila hata nje ya mipaka.

Wakati huo huo, Tanzania na India zimetia saini hati za makubaliano 14 na mkataba mmoja ambapo hati 10 zimehusisha taasisi za serikali na hati tano zinahusisha sekta binafsi.

Licha ya kuwa tayari India inasaidia Tanzania katika masuala ya ubobezi wa kupandikiza figo na uboho (Born marrow) pia viongozi hao wamejadili namna ya kuanzisha kituo cha dawa asili.

Aidha, masuala mengine yaliyojadiliwa katika ziara hiyo ni usalama mtandaoni, kushirikisha vijana hasa kupitia vyuo vya VETA kutoa mafunzo kwa wahandisi wa madini, kushirikiana kwenye kilimo na miradi ya maji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *