Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wizara ya Ujenzi kupitia wakala wa Barabara (TANROADS) imejipanga kukabiliana na majanga ya asili kama mafuriko katima maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo yanayokumbwa na mafuriko ya mara kwa mara kwa lengo la kuimarisha miundombinu kwa kuijenga yenye uwezo wa kuhimili mafuriko yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Akihutubia Bunge wakati wa kuwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2025/26, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega, amekiri kuwa uwezo wa baadhi ya madaraja na barabara kuhimili vishindo vya mabadiliko ya tabianchi ni mdogo, akisisitiza mpango wa wizara yake katika ujenzi wa madaraja na barabara zenye kuzingatia mahitaji ya kisasa ya dunia.
Aidha, Waziri ulega ameeleza kuwa serikali itaendelea kuimarisha kituo chake cha kukabiliana na dharura za majanga (Emergency Response Centre) kilichopo kwenye Ofisi za TANROADS mkoa wa Pwani, kituo hicho kikifanya manunuzi ya vifaa mbalimbali vya kukabiliana na dharura ikieemo makalavati ya chuma yenye urefu wa Mita 5,750, nyavu za kushikilia mawe kwenye kingo za madaraja na magodoro yake yenye jumla ya Mita za ujazo 4,500 vyote vikigharimu Sh. bilioni 4.91.
Aidha, Waziri Ulega ameeleza kuwa sambamba na uimarishaji na uanzishaji wa vituo vingine vya kukabiliana na majanga ya asili, wizara yake kupitia TANROADS inaboresha miongozo ya usanifu wa vifaa vya ujenzi (Building Material) ili kuhakikisha miundombinu mipya inayotengwa inahimili mabadiliko ya tabia nchi.
Ulega amesema mojawapo ya changamoto kubwa ambayo imeikumba sekta ya ujenzi kikanda na Kimataifa katika miaka ya karibuni ni suala zima la mabadiliko ya tabianchi, akitaja ongezeko la vimbunga na mvua kubwa zinazosababisha mafuriko yasiyokuwa ya kawaida kama changamoto kuu ya ujenzi.
