Tanroads inavyojitahidi kuimarisha miundombinu ya barabara Tabora

Na Benny Kingson, Tabora

MKOA wa Tabora una mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 2,188.09 zinazohudumiwa wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Meneja Tanroads Mkoa wa Tabora, Mhandisi Raphael Mlimaji, anasema kuwa, kati ya hizo, kilometa 967.09 ni za Barabara Kuu na km 1,158.01 ni za Barabara za Mkoa na km 62.99 za Wilaya.

Anasema, km 794.67 za Barabara Kuu ni za kiwango cha lami, wakati km 172.42 ni za changarawe.

Kwa upande wa Barabara za Mkoa, km 53.74 ni za lami na km 1,104.27 ni za changarawe au udongo.

Kwa ujumla, Tanroads imefanikiwa kuimarisha miundombinu yote ya barabara na kuufanya mkoa kuunganishwa kwa urahisi.

“Kilometa 3 katika Barabara za Wilaya ni za kiwango cha lami, hii ni Barabara ya Igunga – Mbutu, na km 59.99 ni za changarawe au udongo. Hizi zimekasimiwa na Wakala ya Barabara katika Mkoa wa Tabora,” anafafanua.

Mhandisi Mlimaji anabainisha kuwa, Tanroads mkoani humo inahudumia jumla ya madaraja 611 yaliyojengwa kwenye mtandao huo wa barabara.

Matengenezo ya barabara na madaraja

Anasema, kila mwaka kuanzia Mwaka wa Fedha 2020/21 mtandao huo wa barabara zenye urefu wa jumla ya km 2,188.09 ulipokea matengenezo mbalimbali ya barabara na madaraja pamoja na ukarabati.

“Mpaka kufikia mwaka 2022/23 jumla ya Shs. bilioni 76.060 zilitumika kulipia kazi hizo,” anasema.

Katika Mwaka wa Fedha 2023/24 kiasi cha Shs. bilioni 25.641 kimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara na madaraja pamoja na ukarabati wa barabara sehemu zilizochakaa zaidi,  hiyo inahusisha km 2,329.65 za barabara na madaraja 40.

Miradi iliyotekelezwa 2021 – 2023

Miradi ya barabara inayotekelezwa ni pamoja na barabara ya Tabora – Sikonge – Mpanda (km 363), Tabora – Nyahua – Chaya (km 170), na Kazilambwa – Chagu (km 36).

Pia ujenzi wa kipande cha km 26 za barabara ya Kaliua-Malagarasi-Ilunde yenye urefu wa km 156 unaendelea.

Kwa upande mwingine, kwenye barabara ya Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa kilometa 36, km 26 kati ya hizo zipo Mkoa wa Tabora na km 10 zipo Mkoa wa Kigoma.

Mhandisi Mlimaji anasema, ujenzi wa barabara hiyo ulianza kwa kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2009 na Mhandisi Mshauri Ms Crowntech Consult Ltd ya Dar es Salaam kwa gharama ya Shs. 134,423,076.92.

“Mnamo 3/8/2020 ujenzi wa barabara hii ulianza kutekelezwa ukiwa unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100%. Mwaka 2021 ulipata mfadhili ambaye ni Mfuko wa Miradi ya Maendeleo Kimataifa “OPEC Funds” wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 26,” anaeleza.

Mfadhili huyo amegharamia ujenzi wote huku Serikali ya Tanzania ikichangia kiasi cha Dola milioni 1.5 kulipia gharama za upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na fidia kwa wananchi 199 waliopisha eneo la mradi.

Mhandisi Mlimaji anasema, wananchi wa vijiji vya Ugansa na Malanga waliopisha mradi walilipwa fidia ya jumla ya Shs. 725,381,900. Mradi huo umesimamiwa na Tanroads Engineering Consulting Unit (TECU).

Aidha, kiasi cha Shs. 1,609,465,299.00 kililipwa kama mishahara na posho kwa wafanyakazi waliotekeleza kazi ya ujenzi kuanzia mwaka 2020 mpaka mradi unakamilika Septemba 2023.

Mhandisi Mlimaji anaeleza kuwa, mradi huo umeshakamilika kwa asilimia 99 na kazi zinazoendelea ni ndogondogo za kukinga madaraja yasije kusombwa na mvua kwa kujengea na mawe pembeni (grout stone pitching).

Meneja huyo anataja kazi zilizofanyika hadi Sesptemba 2023 kuwa ni pamoja na ujenzi kambi ya mkandarasi 100%, ujenzi kambi ya Mhandisi Mshauri 100%, kusafisha eneo la barabara km 33.8 (100%) na kuondoa udongo wa juu (top soil) km 33.8 (100%).

Kazi nyingine zilizofanyika ni kujenga tabaka la kwanza la barabara G3 km 33.8 (100%), tabaka la pili la barabara G7 km 33.8 (100%), tabaka la tatu la barabara G15 km 33.8 (100%).

“Kazi nyingine zilizokwisha fanyika ni ujenzi wa kalvati za bomba 36 (100%), ujenzi wa kalvati za access 25 (100%) na ujenzi wa boksi kalvati 9 (100%).

“Kazi nyingine ni ujenzi wa tabaka la saruji km 33.8 (100%), ujenzi wa tabaka la kokoto (CRR) km 33.8 (100%), ujenzi wa tabaka la kwanza la lami km 33.8 (100%), ujenzi wa tabaka la pili la lami km 33.8 (100%), kuweka alama za barabarani (100%), kujengea mawe pembeni ya makalvati (99%) na kazi zote kwa ujumla zimekamilika kwa asilimia 99,” anabainisha.

Mhandisi Mlimaji anaeleza kuwa, malipo ya awali ya asilimia 15 ya gharama za mradi Shs. bilioni 4.632 yalifanyika Mei 5, 2021 na Hati za Malipo Na. 1 – 20 zilizoidhinishwa hadi Septemba 30, 2023 ni Shs. bilioni 22.727.

“Kiasi kilicholipwa Shs. bilioni 22.65 na kiasi cha Shs. milioni 77.285 hakijalipwa ingawa kuna kazi ambazo mkandarasi bado hajaomba malipo yake mpaka sasa zimeshafanyika,” anasema.

Meneja huyo wa Tanroads Mkoa wa Tabora anasema kuwa, wakati wa kuanza kwa mradi kulikuwa na changamoto ya kucheleweshwa kwa malipo ya awali ambapo yalichelewa kwa takribani mwaka mzima, changamoto hiyo na mkandarasi akalipwa.

Changamoto nyingine inatajwa kuwa ni kuchelewa kupata Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT Exemption) ambayo ilichangia kuchelewa kwa mradi kutokana na mlolongo mrefu (hii ilikuwa ni mwanzoni mwa utekelezaji wa mradi), lakini changamoto nyingine ni wizi wa alama za barabarani.

Mhandisi Mlimaji anasema, kazi nyingine zinazotekelezwa na Tanroads Mkoa wa Tabora ni ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege (Jengo la abiria, maegesho ya magari, uzio na barabara za maingilio. Ikumbukwe kuwa, Mkoa waTabora una kiwanja cha ndege kimoja ambacho ndicho kinachoboreshwa kiweze kuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja.

“Ujenzi wa Uwanja wa Ndege unahusisha ujenzi wa jengo lenye gorofa mbili, jengo la chini na la kwanza (Ground and First Floor) ni kwa ajili ya abiria wanaoondoka na kuingia na ghorofa ya pili ni kwa ajili ya kuongozea Ndege (Control Tower),” anaeleza.

Kulingana na meneja huyo, ujenzi huo utahusisha ujenzi wa uzio wa uwanja wa ndege sehemu zilizo wazi km 6.5 na ujenzi wa maegesho ya magari yenye uwezo wa kuegesha magari 54 kwa wakati mmoja.

Gharama za mradi huo, anasema, ni Shs. 27,032,172,956, ambapo mkataba ulisainiwa Juni 20, 2017 ukiwa ni mkataba Namba AE-027/2016-2017/TBR/25 chini ya Msimamizi Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Hata hivyo, mkataba huo umeanza kutekelezwa tarehe 1/4/2023 baada ya marekebisho ya kimkataba kufanyika ikiwa ni mabadiliko ya Msimamizi wa Mradi, ambapo sasa Tanroads ndiye msimamizi mkuu, ukiwa unafadhiliwa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na mkandarasi ni kampuni ya Beijing Construction Eng. Group ya China.

Inaelezwa kuwa. Utekelezaji wa mradi huo umefikia 6.80% ambapo hadi kufikia Septemba 30, 2023, kazi zilizofanyika ni ujenzi kambi ya mkandarasi 100%, uchimbaji wa msingi wa jengo 100%, ujenzi wa nguzo za msingi 60%, ujenzi wa ukuta wa msingi 30%, ujenzi wa uzio ni 5%, ujenzi wa maegesho ya magari ni 0% na ujenzi unaendelea.

Aidha, malipo ya awali ya asilimia 15 ya gharama za mradi Shs. bilioni 4.055 yalifanyika tarehe Agosti 4, 2022.

Meneja huyo anataja changamoto katika mradi huo kuwa ni kuchelewa kuanza kwa utekelezaji kulikosababishwa na kuhamishwa kwa wasimamizi wa Mradi kutoka TAA kwenda Tanroads ambako kulisababishwa na mabadiliko ya Makubalian ya Mkopo (Loan Agreement).

Anataja changamoto nyingine ni kubadilika kwa bei, kwani mkataba ulisainiwa mwaka 2017 na mradi umeanza mwaka 2023.

Ujenzi wa miradi inayosimamiwa na Mkoa

Utekelezaji unaosimamiwa na Tanroads Mkoa wa Tabora ni pamoja na mradi wa barabara ya Ushokola – Kaliua – Kasungu km 5.5 (Ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano), ambayo mpaka sasa urefu uliotekelezwa ni km 4.1. Jumla ya taa za barabarani 110 zimewekwa.

Barabara nyingine ni Ulyankulu – Kaliua km 3 (Ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano), ambapo mpaka sasa kilometa 2.8 zimekwishajengwa na jumla taa 44 za barabarani zitawekwa.

Barabara nyingine ni Sikonge – Mibono – Kipili (Sikonge Mjini) km 8, ambayo mpaka sasa kilometa 3.865 zimejengwa. Pamoja na ujenzi wa Barabara ya Ipole-Rungwa (km 172.4).

“Wakati Serikali inaendelea Kutafuta fedha, tayari tumekwishaanza kujenga Daraja la Msuva lenye urefu wa mita 10 na barabara ya maingilio ya km 0.60 kiwango cha lami na kunyanyua tuta lenye urefu wa km 2.0. Gharama za Mkataba ni Shs. bilioni 1.651,” anaeleza.

Mradi huo ambao unatekelezwa na Mkandarasi Salum Motor Transport Co. Ltd, umefikia 8.0%. mpaka sasa huku kazi zilizotekelezwa hadi Septemba 30, 2023 zikiwa ni kusafisha eneo la barabara km 1.0 (100%), uchimbaji wa sehemu ya kujenga daraja m 11 (100%), kuweka mawe (100%), kazi ya nzege (blinding) (100%), kufunga nondo kwenye msingi (75%) na kazi zinaendelea kwa ufanisi mkubwa sana.

Mlimaji anasema, hakuna malipo yoyote yaliyolipwa hadi sasa.

Mradi mwingine ni ujenzi wa barabara ya Mambali-Bukene-Itobo (km 114) kwa kiwango cha lami, ujenzi wa km 1.0 umeanza wakati serikali ikiendelea kutafuta fedha zitakazojenga kilometa zote hizo kwa gharama ya Shs. bilioni 1.001. Mkandarasi katka mradi huo ni kampuni ya Salum Mtor Trasport Co. Ltd anayetakiwa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo katika kipindi cha miezi 10.

Kazi zilizofanyika hadi kufikia Septemba 30, 2023 ni kusafisha eneo la barabara km 1.0 (100%), kuondoa udongo wa juu (top soil) km 1.0 (100%), tabaka la kwanza la barabara G3 km 1.0 (100%) na tabaka la pili la barabara G7 km 1.0 (5%). Mkandarasi huyo bado hajalipwa malipo yoyote mpaka sasa.

Mradi mwingine unaoendelea kutekelezwa ni ujenzi wa barabara ya Nzega – Kagongwa (km 66) ambapo katika Mwaka wa Fedha 2023/24 kiasi cha Shs. bilioni 2.5 kilitengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi, ambapo Tanroads makao makuu ndio wanafanya manunuzi.

Mhandisi Mlimaji anasema, pia wanaendelea na zoezi la kuweka taa za barabarani mkoani humo ambapo jumla ya taa 3,279 zimewekwa katika barabara na wataendelea kuziweka kadiri ya fedha zinavyotolewa kwa lengo la kuongeza usalama barabarani nyakati za usiku kwa watumiaji wa barabara.

“Pia tuna jumla ya taa nne (4) za kuongozea magari na watembea kwa miguu, kuna taa tatu (3) za kuongozea watembea kwa miguu maeneo ya Igunga kwa ajili ya kuongeza usalama kwa wavuka barabara kwa miguu,” anaeleza.

Miradi ya usanifu yakinifu na usanifu wa kina inayoendelea

Mhandisi Mlimaji anaeleza kuwa, katika mwaka wa fedha 2023/24 Tanroads Mkoa wa Tabora idhinishiwa jumla ya Shs. bilioni 215 kutekeleza miradi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika barabara mbalimbali zenye jumla ya km 293 na kwamba miradi mitatu (3) itafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Anaainisha kazi hizo kuwa ni upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Puge-Ziba-Choma (km 109) Sh. bilioni 45.

Meneja huyo anataja kazi zilizofanyika kuwa ni upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara ya Mambali-Bukumbi- lshihimulwa-Shitage Kahama (km 105) – TShs. 55.000 milioni na unasubiri kutangazwa robo ya pili ya mwaka.

Kazi nyingine ni upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara ya Tabora-Ulyakulu (km79) Shs. bilioni 115 unasubiri kutangazwa robo ya pili ya mwaka.

Utekelezaji ahadi ya Rais Samia

Mhandisi Mlimaji anaeleza kuwa mnamo Mei 15, 2023, Rais Samia alikuwa katika viwanja vya Stendi ya Tura aliahidi ujenzi wa Daraja la Loya. Hatua ya utekelezaji wa ahadi hiyo ni usanifu wa kina ambao umekamilika.

“Kiasi cha Shs. bilioni 27.40 kinahitajika kutekeleza ahadi ya Rais Samia na hatua inayofata ni ujenzi baada ya kupewa kibali cha kuanza ujenzi na kupewa fedha,” anabainisha.

Anahitimisha kwa kueleza kuwa Tanroads imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuifanya miundimbinu ya barabara za mkoa huo zimekuwa katika hali nzuri na bora wakati wote na anahakikisha ataendelea kuwajibika kwa bidii zaidi kwa kuzingatia ni mzawa wa mkoani Tabora.

Meneja huyo ambaye amethibitishwa hivi karibuni kutumikia wadhiwa huo ambao amekuwa akikaimu nafasi hiyo ameonyesha kuwakonga nyoyo wabunge wa mkoani humo na kukubalika kutokana na utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *