TANESCO yaajiri watumishi wapya 555 kwa wakati mmoja


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeandika historia kwa kuajiri watumishi wapya 555 kwa mara moja.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Dkt. Rhimo Nyansaho, ameyasema hayo leo jijini Dodoma katika uzinduzi wa mafunzo elekezi kwa waajiriwa hao.



Mafunzo hayo yalifunguliwa Julai 21, 2025 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, yakilenga kuwapa uelewa mpana kuhusu majukumu yao ndani ya Utumishi wa Umma na ndani ya Shirika, kabla ya kuanza kazi rasmi katika maeneo waliyopangiwa kote nchini.



Akifungua mafunzo hayo, Dkt. Nyansaho aliwataka watumishi hao wapya kutambua uzito wa fursa waliyoipata na kuitumikia kwa bidii, uadilifu na uaminifu mkubwa.

“Kipekee namshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia kibali cha kuajiri. Hii ni fursa ya kipekee na ni wajibu wenu kuithamini kwa kufanya kazi kwa juhudi na weledi mkubwa,” amesisitiza Dkt. Nyansaho.

Amewaasa kuhusu mwenendo wao wa kikazi, aliwakumbusha kuwa TANESCO imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma bora kwa wateja, hivyo wanapaswa kuendeleza juhudi hizo kwa kuwahudumia wateja kwa kuwajibika na kuwa na maadili ya hali ya juu.

“Tumepiga hatua kwenye utoaji wa huduma bora kwa wateja, hivyo ni muhimu mwendeleze kwa kuwahudumia wateja kwa uaminifu na uadilifu kwa maslahi mapana ya Shirika na Taifa kwa ujumla,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, aliwataka waajiriwa hao kuwa mabalozi wa Shirika katika maeneo yao ya kazi kwa kutekeleza majukumu yao kwa bidii, uaminifu na kwa kutoa huduma bora kwa wateja.

“Katika majukumu yenu, mnakwenda kukutana na wateja wetu. Wahudumieni kwa heshima na kwa moyo wa kujitolea, ili kwa pamoja tuendelee kujenga taswira chanya ya TANESCO,” ameeleza Twange.

Waajiriwa hao wameajiriwa na TANESCO hivi karibuni baada ya kupitia mchakato wa ajira, huku awali wakiwa wafanyakazi wa mikataba ya muda na ajira hizi mpya zinawapa fursa ya kupata ajira za kudumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *