Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na wadau, wamewataka waathirika wa rushwa ya ngono, unyanyasaji kijinsia mahala pa kazi kupaza sauti zao ili wapate msaada.
Wadau hao ni pamoja na Mfuko wa Udhamini Wanawake Tanzania (WFT-T) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Rose Reuben, aliyasema hayo Dar es Salaam jana.
Alisema tatizo la rushwa ya ngono sio la kunyamaziwa kwa sababu linaua ndoto na kuchelewesha malengo ya wanawake na watoto wa kike nchini.
Aliiomba serikali kulichukulia kwa uzito suala la kuwawajibisha watu wote wanaoomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi, wafanyakazi ili kulinda haki zao.
Alieleza kuwa, miaka mitano mfululizo TAMWA imetekeleza mradi wa kuchapisha habari za uchunguzi juu ya rushwa ya ngono wakishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo WFT-T , TAKUKURU na wanamtandao wa kupinga ukatili wa kijinsia nchini.
Reuben alisema Novemba 25 kila mwaka, wataanza safari ya siku 16 za kupingwa ukatili wa kijinsia ili kukumbusha jamii kuwa ukatili wa kijinsia ni mchakato unaofanyiwa kazi kila siku, unaohitaji utashi wa jamii ili kutekeleza.
“Mwaka huu, TAMWA katika kuadhimisha maadhimisho hayo tumewekeza kupinga rushwa ya ngono, unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya kazi, taaluma yetu kupinga unyanyasaji huo katika vyumba vya habari, wanahabari ikiwamo kwenye shule za habari,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa WFT-T, Rose Marandu alisema rushwa ya ngono imekuwa ikiangusha ndoto za watu wengi, inadhalilisha na kuua.
Alisema pia imekuwa inaleta madhara makubwa kwa jamii, kusababisha watu kukosa amani ambapo kesi zake mara nyingi hupelekwa katika makosa ya uhujumu uchumi.
Mchunguzi Mkuu wa PCCB, Dorothea Mrema, alisema kwa mujibu wa makosa yote yaliyopo katika sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya Mwaka 2007, yapo makosa 24 lakini kosa moja pekee lipo kifungu cha 15 la kuhonga na kupokea ndilo halipo katika sheria ya uhujumu uchumi, mengine yapo katika uhujumu uchumi.
“Ni ukweli uhujumu uchumi adhabu yake ni kuanzia miaka 20 na kuendelea, makosa yote ikiwemo rushwa ya ngono yanahusishwa na sheria ya uhujumu uchumi,” alisema.