WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amesema hadi Machi, 2025 Sh.Trilioni 1.11 zimekusanywa sawa na asilimia 93.15 ya lengo la kukusanya Sh.Trilioni 1.60 kwa Mwaka 2024/25.
Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi hiyo kwa Mwaka 2025/26, Waziri Mchengerwa amesema kati ya fedha hizo Sh.Tilioni 61.21 ni kodi ya majengo, Sh. Trilioni 1.04 ni mapato ya ndani ya mamlaka za serikali za mitaa.Pia, amesema Sh.Bilioni 16.23 ni mapato ya ndani ya taasisi na Sh.Milioni 201.60 ni maduhuli ya mikoa.Amefafanua kuwa makusanyo hayo yalitokana na ada za wanachuo, tozo, ukusanyaji wa madeni, mauzo ya bidhaa mbalimbali na ushuru unaotozwa na mamlaka za serikali za mitaa kulingana na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290.

Mchengerwa amesema kwa kipindi hicho TAMISEMI ilipanga kutumia Sh. Bilioni 541.27 za mapato ya ndani ya halmashauri kwaajili ya kuchangia utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Hadi Machi, 2025 Sh.Bilioni 312.30 sawa na asilimia 57.70 zimetolewa.
Ameeleza kuwa baadhi ya miradi iliyotekelezwa kwa kipindi hicho ni ujenzi wa miundombinu ya elimu, afya, ujenzi wa barabara, machinjio, minada nyumba za walimu na watumishi wa afya, hospitali, vituo vya afya, zahanati, vituo vya polisi, ununuzi wa magreda.

