Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
JUMUIYA ya Kampuni za Uwindaji wa Kitalii Tanzania (Tanzania Hunting Operators Association-TAHOA) imetoa salamu za pole kwa waathirika wa maafa ya marufiko ya tope, Hanang, mkoani Manyara.
Mafuriko hayo yamesababisha vifo, majeruhi, uharibifu mkubwa wa miundombinu na mali.
Salamu za pole zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa TAHOA, Abdulkadir Mohamed wakati akikabidhi mchango wao kwa waathirika wa maafa hayo.
Alisema jumuiya hiyo imetoa mchango wa fedha za kununua vifaa vya ujenzi vyenye gharama ya sh. milioni 47,409,800 ambavyo vitapelekwa Hanang.
“Sisi kwa umoja wetu tumechanga fedha za ununuzi vifaa vya ujenzi ambavyo vitapelekwa Hanang.
“Tumeungana na Serikali kwa kukabidhi mchango wetu utakaosaidia wananchi wa Katesh-Hanang kurejesha hali zao za maisha katika ubora zaidi,” alisema Abdulkadir.
Akitoa neno la shukrani baada ya kupokea msaada huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, aliishukuru TAHOA kwa namna walivyojitoa kuungana na Serikali ambapo kazi kubwa iliyopo ni kurejesha hali hasa makazi kwa wana Hanang.
“Mmekuja wakati sahihi kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo ni vifaa vya ujenzi, mmeleta msaada huu ambao utasaidia vitu muhimu vinavyohitajika kwa ujenzi ikiwemo saruji ambayo itasaidia kupata makazi salama na sahihi kwa Wana Hanang,” alieleza Mhagama.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki aliwashukuru TAHOA kwa kuonesha utayari wao wa kuchanga kwa ajili ya waathirika wa maafa ya Hanang.
Alisema zoezi lote limefanikiwa kutokana na uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuungana na Watanzania waliofikwa na maafa hayo.
“Kipekee nikupongeze Waziri mwenye dhamana ya uratibu, Mhagama kwa namna ulivyolisimamia hili na kuhakikisha hali za wakazi wa Hanang zinarejea, hakika mmefanya kazi kubwa kwa maelekezo ya Rais wetu,” alisisitiza Kairuki.
TAHOA inajumuisha wanachama kutoka Kampuni za Robin Hurt Safaris Ltd, Tanzania Big Game Safari Ltd, Tanzania Safaris and Hunting Ltd, Safari Royal Holding Ltd,EBN Hunting Safaris Ltd, African Buffulo Safaris Tracers, Michel Mantheakis Safaris Ltd.
Luke Samaras Safaris Ltd, Pori Trackers of Africa Ltd, Bushman Safaris Trackers Ltd, Game Frontiers of Tanzania Ltd, Rungwa Game Safaris Tanzania.
Eshkesh Safari Ltd, Mwatisi Safaris Ltd, Ilaroi Ranching Ltd, Tanzania Game Trackers Safari Ltd na Transports Costings.