
RAIS wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo na Vyuo Vikuu nchini Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba, amemshukuru Rais wa Awamu ya Sita nchini Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji wake mkubwa katika sekta ya elimu ya Vyuo na Vyuo Vikuu nchini, akisisitiza kuwa Jumuiya hiyo itakuwa mstari wa mbele kueleza kwa Watanzania yale yote yaliyofanyika kwa Miaka minne ya serikali yake.
Kiliba ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 24, 2025 wakati wa Kongamano la Vyuo na Vyuo Vikuu nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 Jijini Dar es Salaam akimshukuru pia kwa kutunisha mfuko wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya Juu kutoka Bilioni 464 hadi kufikia zaidi ya Bilioni 960, akisema ongezeko hilo linadhihirisha mchango wa Dkt. Samia katika kutambua umuhimu wa elimu.
“Tunamshukuru sana Mama yetu Dkt. Samia kwanza kwa kutuona, kutujali na kubeba upendo wa Mama. Hakuona kuna shida ama ugumu wowote katika kutuongezea bajeti ya mikopo. Huyu ni kiongozi anayejua umuhimu wa elimu na mara zote ameboresha mazingira yetu ili kusoma katika mazingira bora ili kuja kuwa rasilimali na nguvu kazi bora kwa Taifa letu.” amesema Kiliba.
Kiliba pia amemshukuru Dkt. Samia kwa kazi kubwa inayoendelea kote nchini ya kujenga Matawi ya Vyuo Vikuu kwenye mikoa mbalimbali nchini hasa ile ya pembezoni, akisema Matawi hayo yamesaidia na yatasaidia kuendelea kutoa fursa za elimu na kusogeza huduma hiyo karibu zaidi na vijana badala ya kusafiri kwenda Dar es Salaam kuifuata elimu ya vyuo na vyuo vikuu.
Aidha, katika hatua nyingine Kiliba amemwombea kheri Dkt. Samia katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 29, 2025, wakiahidi kuwa mabalozi wema wa kazi kubwa iliyofanywa kwa Watanzania katika kipindi chake cha Miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.




