TADB yawashika mkono wahitimu ‘waliotusua’ SUA

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imewapongeza wahitimu bora wa Chuo Kikuu cha Kilimo Cha Sokoine (SUA) cha Morogoro kwa kuwapatia zawadi ya fedha taslimu Sh. milioni 5.

Motisha hiyo ya fedha, imetolewa na TADB kama sehemu ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kupitia mpango mkakati wake mpya uliozinduliwa mwaka huu.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri na wafanyakazi katika eneo la utafiti, Ofisa Rasilimali Watu Mkuu wa TADB, Jacqueline Minja, amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Benki yetu inatambua uwapo wa mikakati mbalimbali ya serikali kama vile sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 ambayo imetilia mkazo umuhimu wa kuweka mazingiza wezeshi kwa vijana kujihusisha na shughuli za kiuchumi, ikiwemo kilimo cha kisasa na kibiashara. Kwa kutambua hili, kwa kuanza, TADB imefika hapa na kutoa tuzo kwa wanafunzi bora mwaka huu,” amesema.

Amesema katika awamu nyingine, benki itaandaa programu maalumu ya kuatamia vijana bora kutoka SUA ilikutoa fursa ya kujifunza kazini.

“Programu hiyo itakayokuwa ya miezi 24, italenga kutoa nafasi kwa wahitimu bora kupata nafasi ya kujifunza kazi kwa vitendo katika benki yetu,” ameeleza Minja.

Akizungumza katika mahafali hayo, Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Prof Raphael Chibunda, aliishukuru TADB kwa kutoa motisha kwa wanafunzi wanaofanya vizuri pamoja na mpango wake wa kuandaa programu maalum ya kuwaatamia wahitimu wa fani ya kilimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *