
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini Tanzania Tanzania TARURA, Injinia Victor Seff, ameeleza kuwa kukamilika kwa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania, kwa Awamu ya Pili TACTIC kwa Jiji la Arusha kutabadilisha mwonekano na mandhari ya jiji hilo kuendana na hadhi yake ya mkoa wa kitalii, kuongeza fursa za ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha hali ya biashara na hivyo pia kuchangia maendeleo ya kijamii.
Injinia Seff alibainisha hayo jana Ijumaa Mei 2, 2025 mbele ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mohammed Mchengerwa, kwenye kituo kidogo cha daladala Kilombero, wakati wa utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo utakaohusisha Ujenzi wa kituo kikuu cha Mabasi Bondeni city, Ujenzi soko kuu la Kilombero, Ujenzi soko la Morombo pamoja na uboreshaji wa bustani ya mapumziko ya Themi Living Garden, miradi itakayotekelezwa na mkandaradi M/s Mohammed Builders Limited kwa gharama ya Sh. trilioni 30.6 bila ya VAT.

Kulingana na Mhandisi Seff kukamilika kwa Kituo kikuu cha Mabasi Jiji la Arusha kutawezesha uwapo wa vibanda vya wafanyabiashara 900 kutoka 250 vya sasa, mifumo ya ulinzi kwa kutumia Camera za CCTV, maegesho ya magari pamoja na huduma nyinginezo, zitakazowezesha makusanyo kuongezeka kutoka milioni 72 kwa Mwezi hadi Sh. Milioni 260.
Aidha, kukamilika kwa ujenzi wa Soko la Kilombero, mbali ya kubadilisha mwonekano wa Jiji la Arusha, soko hilo litakuwa na Vibanda 3,274 kwaajili ya wafanyabiashara na wajasiriamali pamoja na huduma nyinginezo za ulinzi kwa kutumia kamera za CCTV, huku soko la Morombo likiwekwa vibanda 752 kutoka vibanda 587 vya sasa na hivyo kuchangia kwenye makusanyako ya Jiji kufikia jumla ya Sh. milioni 117 kwa mwezi kwa masoko yote mawili.

Kuhusu bustani ya Themi, Mhandisi Seff ameeleza kuwa eneo hilo litakuwa na maeneo rasmi ya kupumzikia kwa faragha mbalimbali, mfumo rasmi wa uendeshaji, huduma za vyakula, viburudisho na burudani. maegesho mbalimbali, vyoo na huduma za kujisitiri kwa wanawake, bustani za miti na maua pamoja na ulinzi wa kamera za CCTV.


