Suluhu hana suluhu na wazembe

Na Daniel Mbega

LEO naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuongeza mwaka mwingine katika maisha yangu. Naonekana kama nina miaka 21, najihisi kama ndiyo kwanza nina miaka 18, lakini najitahidi kutenda na kuwajibika kama kijana wa miaka 10 (enzi zile baba yangu ananituma nikachunge ndama), hii inanifanya leo hii nifikishe miaka 49! Naam. Imenichukua miaka 49 kuwa hivi nilivyo. Naamini kwa rehema za Mungu nitafikisha nusu karne mwaka ujao. Happy birthday to me!

Katika kipindi cha uhai wangu nimeshuhudia tawala za marais wote sita tangu kupata Uhuru – kuanzi Mwalimu Julius Nyerere, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Ben Mkapa, Jakaya Kikwete, John Magufuli na sasa Mama Samia Suluhu Hassan.

Katika kipindi hicho nimeona mabadiliko mengi ya uongozi ndani ya Serikali, ambayo yote yalilenga kuboresha utendaji na kuwaletea wananchi maendeleo.

Niliona, wakati huo niko shule ya msingi, jinsi Mwalimu Nyerere na Waziri Mkuu wake Edward Moringe Sokoine, walivyowashughulikia wahujumu uchumi na walanguzi.

Watendaji wa serikali ambao ama walishindwa kuwajibika au waikwenda kinyume na maadili walishughulikiwa kimya kimya. Pengine kwa kuwa wakati huo hakukuwa na utandawazi kama ilivyo sasa. Tulikuwa tunasikia tu kwamba “Fulani amestaafishwa kwa manufaa ya umma!”

Lugha hii ilitumika pia hata katika awamu ya pili na ya tatu. Hakukuwa na “wambeya” kama ilivyo sasa ambapo hata jambo la jikoni unaweza kulikuta kesho mtandaoni! Maadili yalizingatiwa sana, hata “waliostaafishwa kwa manufaa ya umma” nao hawakuropoka hovyo kama hawa wa sasa.

Leo hii mtu ameteuliwa, lakini akitenguliwa anakuwa ndiye chanzo cha kuvujisha siri kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuna hili na lile. Anasahau hata kiapo cha utumishi alichokula wakati akikabidhiwa madaraka – kwamba hatatoa siri kamwe!

Sawa. Katika awamu ya tano kaulimbiu ya “waliostaafishwa kwa manufaa ya umma” ilibadilika na kuwa “kutumbuliwa”. Hii ni kwa sababu ya kaulimbiu ya “kutumbua majipu” iliyokuwepo wakati huo.

Na kusema kweli katika awamu hiyo ndipo tulishuhudia ‘kuteuliwa na kutumbuliwa’. Hata walioteuliwa walikuwa na hofu ya nafasi zao. Siku ikimalizika walikuwa wanapumua, lakini hawakuwa na uhakika kama asubuhi wakiamka bado wanaweza kuwa katika nafasi zao, kwani wangeweza kutumbuliwa hata usingizini!

Sasa tuko ndani ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na sijaipata vyema kaulimbiu inayotumika kuelezea wale wanaotenguliwa nafasi zao za uongozi.

Ndiyo. Naye amefanya mabadiliko mengi tu kwenye serikali yake kwa kuteua na kutengua na hata kuwabadilisha wateule hao ili kuleta ufanisi wa utendaji. Hili linafanywa na viongozi wote ulimwenguni na wala siyo jambo geni.

Lakini kilicho wazi ni kwamba, Mama Samia, ambaye aliapishwa kuwa Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kifo cha JPM, ameikuta nchi ikiwa katika kipindi kigumu.

Kwanza, kwa kuwa aliingia baada ya uchaguzi, ilikuwa vigumu kwake kupanga safu yake ya uongozi, tofauti na kama angefanya hivyo wakati wa kugombea uongozi na kuchaguliwa. Baraza la mawaziri alilirithi kutoka kwa mtangulizi wake na kwa maana nyingine alikuwa na kila sababu ya kubadili hapa na pale ili kuhakikisha anaowaweka kwenye nafasi husika wanamsaidia katika azma yake ya kuwaletea Watanzania maendeleo.

Hata watendaji wengi waliokuwa serikalini ambao tulidhani wana uadilifu mkubwa na wawajibikaji, tukaja kugundua baadaye kuwa kumbe walikuwa na ‘nidhamu ya woga wa kutumbuliwa’ katika utawala uliopita.

Baadhi yao miongoni mwa waliobahatika kusalia kwenye utawala huu, ‘wakajisahau’ na kuzembea, wengine wakaanzisha majungu na kuchongeana, wengine wakaanza kulumbana ndani ya ofisi moja – waziri na katibu mkuu, mkuu wa mkoa pengine na katibu tawala, mkuu wa wilaya na mkurugenzi wake, na kadhalika.

Ndiyo maana, Januari 2022 wakati akiwaapisha mawaziri wapya na wale aliowabadilisha wizara, aliwaasa ‘waache muhali’. Kwamba kila mmoja anatakiwa kuwajibika katika nafasi yake.

Jumatatu, Februari 27, 2023 baada ya kuwaapisha wateule wapya kufuatia mabadiliko ya viongozi wakiwemo katika Baraza la Mawaziri aliyoyafanya Jumapili, Februari 26, 2023, Rais Samia alilazimika kufafanua sababu za yeye kufanya mabadiliko mara kwa mara.

Kwanza alisema kwamba, alidhani jeshi lililokuwapo (Baraza la Mawaziri) angekwenda nalo mpaka mwisho wa muhula wake lakini ameeleza kuwa katika safari ajali hutokea.

Kwa hiyo mabadiliko anayoyafanya yanalenga kuongeza ufanisi huku akieleza kuwa wataendelea kunyofoa watu kutoka sehemu mbalimbali watakaoonekana wana akili ili wasaidie serikali.

Lakini jeshi lake alimaanisha pia hata watendaji wengine wakiwemo wakuu wa mikoa na wilaya, makatibu tawala, makatibu wakuu, wakurugenzi na watendaji wengine.

Kwamba, kuna baadhi wanasuguana ndani ya wizara na idara zao ni jambo ambalo liko dhahiri. Kama wakati ule alivyowaasa kwamba hataki muhali, watu wafanye kazi, basi hata sasa hali inaonekana kuendelea hivyo hivyo.

Baadhi wanasuguana kwa kuwa wote ni wateule wa Rais, hivyo wanavimbishiana vifua kwa kusema kwamba ‘aliyewateua ni mmoja’. Lakini wanashindwa kutambua kwamba kuna miongozo ya kazi waliyopewa (job description) inayoelekeza majukumu yao na wapi wanawajibika. Hii tunaida Code of Conduct!

Misuguano hii imesababisha uzembe mkubwa katika kuwatumikia wananchi, jambo ambalo Rais Samia ameliona na kulichukulia hatua. Wananchi wanataka kuona kero zao zinatatuliwa, tena kwa wakati, sasa ‘mafahari wawili au watatu’ wanaposigana kwenye ofisi moja maana yake changamoto za wananchi hazitapatiwa ufumbuzi, hali ambayo itafanya Serikali ‘itukanwe’ na wasioitakia mema.

Hatua alizochukua na anazoendelea kuzichukua Rais Samia ni za muhimu sana kiutawala, kwa sababu “Mchelea mwana kulia, hulia yeye!” Mama Samia hataki kulizwa na wazembe, wala hana sababu ya kutoa machozi. Anajiamini na anaamini misingi ya utawala wake iko imara na inatekelezeka.

Ndiyo sababu hataki kabisa kufanya suluhu na wazembe. Kwanini apate kazi ya kusimama jukwaani ‘kujitetea’ kwa wananchi kwa sababu ya uzembe wa mtu mmoja, tena ambaye yeye mwenyewe alimteua? Haiwezekani.

Binafsi nasema, Rais Samia endelea na msimamo huo huo. Nyofoa wazembe, chomeka wenye utii na uadilifu na waliojawa na uzalendo kwa taifa lao. Umewateua mwenyewe, na unawatengua mwenyewe – haina haja ya kuwafumbia macho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *