Na Zahoro Mlanzi
MSHAMBULIAJI mpya wa timu ya Yanga SC, Hafiz Konkoni, 23, ameanza rasmi maisha mapya ndani timu hiyo kwa kufanya mazoezi ya ‘gmy’ kambini Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Konkoni ambaye amesajiliwa kuziba pengo la Mkongomani, Fiston Mayele anayetajwa kujiunga na Pyramid ya Misri baada ya msimu uliopita kumaliza na mafanikio ya kuwa Mfungaji Bora Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Msimu uliopita katika Ligi ya Ghana, Konkoni, alifunga mabao 15 kwenye mechi 26 na kutoa asisti tatu akimaliza nafasi ya pili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa katika mtandao wa klabu hiyo leo, inaonesha picha za wachezaji mbalimbali wa timu hiyo wakiwa katika mazoezi ya ‘gmy’ kambini kwao Avic Town.
Nyota huyo anakuwa mchezaji mpya wa nane baada ya mabeki Nickson Kibabage kutoka Singida Fountain Gate, Gift Freddy kutoka SC Villa ya Uganda, Kouassi Attohoula Yao, viungo, Peodoh Pacôme Zouzoua wote kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Wengine ni viungo Jonás Mkude kutoka Simba SC, Mahlatse Skudu Makudubela kutoka Marumo Gallants ya Afrika Kusini na Maxi Mpia Nzengeli kutoka AS Maniema Union ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).