Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Michezo ya Kubahatisha ya SportPesa, imewajaza noti klabu hiyo kwa kuipa bonasi ya sh. milioni 405 kwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kutinga hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SportPesa, Tarimba Abbas, amesema wamekabidhi hundi ya thamani ya sh. milioni 405 ikiwa ni sehemu ya makubaliano yaliyokuwepo katika mkataba walioingia na Yanga.
Amesema ni miaka sita sasa tangu wameingia mkataba na Yanga na wanajisikia faraja kuingia mkataba na klabu hiyo ambayo inaipa heshima kubwa nchi kutokana na mafanikio makubwa wanayoyapata.
“Yanga kachukua Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika ilibaki kidogo yanga kutwaa ubingwa wa Shirikisho Afrika kama sio fitna zilizofanyika.” amesema Tarimba.
Tarimba amesema ameridhishwa na mikakati wanayoifanya anatarajia mambo makubwa msimu ujao na wao kama wadhamini wanaona mataji mengine msimu ujao.
Kwa upande wa Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema anawashukuru SportPesa na kuwaahidi wataendelea kuwa wawakilishi wao kwa kufanya yaliyo bora zaidi.
“Mafanikio tuliyoyapata yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na SportPesa kutokana na mkataba wao kuendelea kutekeleza makubaliano yetu yaliyokuwa kwenye mkataba,” amesema Hersi ambaye ametimiza mwaka mmoja tangu ameingia madarakani.