Na Badrudin Yahaya
KLABU ya soka ya Simba, imeingia mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya sh. bilioni 1.5 na Kampuni ya Serengeti Breweries kupitia kinywaji chake cha Pilsner.
Mkataba huo umesainiwa jana jijini Dar es salaam mbele ya Mtendaji Mkuu wa Simba, Iman Kajula na Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti, Obinna Anyalebechi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, CEO wa Simba, Kajula, alisema udhamini huo umekuja wakati muafaka na utasaidia kuchochea maendeleo zaidi ya soka ndani ya klabu hiyo.
Kajula alikiri mpira wa Tanzania kwasasa umekua na hivyo unahitaji fedha nyingi ili kushindana na timu zilizowazidi na kutoa shukrani kwa Serengeti kwa kuamua kuwasaidia katika upande huo kiuchimi.
“Ili tuweze kufanya vizuri tunahitaji fedha nyingi na kwakuwa Serengeti wametuletea fedha hizi basi zitatusaidia katika masuala mbalimbali ya uendeshaji wa klabu yetu,” alisema Kajula.”
Mpira wa sasa uendeshaji wake ni gharama kubwa hivyo tunapopata watu wanaokubali kutushika mkono kama hivi lazima tuwashukuru,” alisema.
Pia Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti, Anyalebechi alisema udhamini huo unatarajia kukuza thamani ya taasisi hizo mbili lakini kubwa zaidi ni kukuza michezo nchini.
Kwa upande wa Meneja Masoko wao, Anitha Rwehumbiza, alisema wamechagua kufanya kazi na Simba kutokana na hamasa na mashabiki waliokuwa nao hivyo haikuwa kazi ngumu kuchagua.
“Haikuwa kazi kubwa kuamua kufanya kazi na Simba, kwanza tunafanana rangi lakini pia klabu hii ina mashabiki wengi ambao wana hamasa nzuri,” alisema.
Mkataba huu umesainiwa kipindi kizuri ambapo Simba wanajiandaa kucheza mchezo wake wa dabi dhidi ya Yanga Jumapili na hivyo hii inatarajiwa kuwa hamasa kubwa kuelekea mchezo huo wa ligi.